Mpango wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Bangladesh, Sheikh Hasina, kurejea nchini humo Desemba 16, 2026, umezua wasiwasi wa kisiasa na kiusalama, huku India ikikabiliwa na changamoto ya kidiplomasia kutokana na ombi la serikali ya Dhaka kumrejesha ili akabiliane na hukumu ya kifo.

Hasina, mwenye umri wa miaka 79, alitangaza kupitia wasaidizi wake kuwa anapanga kurejea Bangladesh katika siku ya maadhimisho ya ushindi wa taifa hilo dhidi ya Pakistan mwaka 1971.

Alikimbilia India Agosti 2024 baada ya maandamano yaliyoongozwa na wanafunzi kusababisha kuanguka kwa utawala wake uliodumu kwa miaka 15.

Hasina alihukumiwa kifo akiwa hayupo mahakamani baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kuhusiana na operesheni ya kukandamiza waandamanaji wakati wa machafuko yaliyomwondoa madarakani.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa hadi watu 1,400 waliuawa na vikosi vya usalama wakati wa maandamano hayo. Hata hivyo, kesi yake imeibua maswali kuhusu haki ya kusikilizwa, huku Hasina akipinga mashtaka dhidi yake.

Serikali ya sasa ya Bangladesh imesema atakamatwa mara moja iwapo atarejea nchini humo na imeahidi kutekeleza hukumu iliyotolewa dhidi yake.

Msemaji wake, Abu Obaidha Arin, amesema Hasina anataka serikali ya Bangladesh impangie safari ya ndege kutoka New Delhi. Iwapo hilo halitawezekana, anaweza kutumia ndege za kawaida au kuingia nchini kupitia mpaka wa nchi kavu.

Arin amesema Hasina yuko tayari hata kutembea kwa miguu kuvuka mpaka kuingia Bangladesh, akisisitiza kuwa mpango huo umeandaliwa kwa umakini.

Hata hivyo, serikali ya Dhaka imesisitiza kuwa kurejea kwake lazima kuwe kwa njia ya kumkabidhi kupitia taratibu za kisheria, huku maafisa wakisema hawezi kuingia nchini kama msafiri wa kawaida.

Kwa upande mwingine, India imesema ombi la Bangladesh la kumrejesha Hasina linafanyiwa tathmini kupitia taratibu zilizopo. New Delhi pia imeeleza kuwa kurejea kwake kwa hiari ni suala tofauti na mchakato wa kumrejesha kisheria.

India inajikuta katika hali ngumu kwa kuwa ilimpa Hasina hifadhi baada ya kuondolewa madarakani, lakini sasa uhusiano wake na Bangladesh umeathiriwa na suala hilo.

Wakati huo huo, chama cha Hasina cha Awami League kimepigwa marufuku nchini Bangladesh, huku wafuasi wake wakiendelea kuhusishwa na maandamano na machafuko katika baadhi ya maeneo.

Wachambuzi wanaonya kuwa kurejea kwake kunaweza kuchochea makabiliano mapya, hasa kutokana na mgawanyiko wa kisiasa na hali ya usalama nchini humo.

Ingawa tarehe ya Desemba 16 imetajwa, safari yake bado haijathibitishwa, huku serikali na wafuasi wake wakiendelea kuwa na misimamo inayokinzana.