Trump Na Katibu Mkuu Wa NATO Wajadili Vita Vya Ukraine Na Iran
Rais wa Marekani Donald Trump amekutana na Katibu Mkuu wa Shirika la Kujihami la NATO, Mark Rutte, katika mazungumzo yaliyolenga vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine pamoja na mzozo wa kijeshi unaohusisha Iran.
Katika mkutano huo uliofanyika faraghani Jumatano, Novemba 25, 2026, viongozi hao walijadili umuhimu wa kuzuia hatua zinazoweza kupanua vita vya Ukraine na kutafuta suluhu ya amani haraka iwezekanavyo.
Kupitia ujumbe aliouchapisha Alhamisi, Trump alisema kuwa katika mazungumzo hayo walijikita katika umuhimu wa Urusi na Ukraine kuepuka vitendo vinavyoweza kuongeza wigo wa mapigano, iwe kwa makusudi au bila kukusudia.
"Tulijadili pia kwa kina umuhimu wa Urusi na Ukraine kuepuka hatua zozote zinazoweza kupanua vita, iwe kwa makusudi au bila kukusudia, pamoja na umuhimu wa kupata suluhu ya amani haraka iwezekanavyo," alisema Trump.
Mazungumzo hayo pia yalihusu hali ya usalama katika Mashariki ya Kati, hususan mzozo unaohusisha Iran, pamoja na namna ya kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi kati ya Marekani na mataifa wanachama wa NATO.
Mkutano huo unafanyika wakati mataifa ya Magharibi yakiendelea kukabiliwa na changamoto za kiusalama zinazotokana na vita vya Ukraine na kuongezeka kwa mvutano wa kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Katika taarifa yake kuhusu mkutano huo, NATO ilisisitiza masuala ya usalama wa pamoja na umuhimu wa kuimarisha uwezo wa kijeshi wa mataifa wanachama.
Hata hivyo, taarifa rasmi ya NATO ilitofautiana kwa kiasi fulani na ujumbe wa Trump kuhusu vita vya Ukraine.
Wakati taarifa ya muungano huo ilisisitiza Urusi kuepuka kupanua vita, Trump alitaja Urusi na Ukraine kwa pamoja.
Rutte amekuwa akihimiza juhudi za kidiplomasia za kumaliza vita hivyo, huku akisisitiza umuhimu wa Marekani na washirika wake kuendelea kushirikiana katika masuala ya usalama.Huenda mkutano huo,ukaleta afueni.
Mkutano huo unaangazia nafasi ya Marekani katika juhudi za kutafuta amani Ukraine, huku pia ukiweka mbele ushirikiano wa kiulinzi katika kipindi ambacho mivutano ya kimataifa inaendelea kuongezeka.









