Kiongozi wa chama cha ODM na Seneta wa Siaya Oburu Oginga amerejea katika shughuli zake za kisiasa baada ya kukabiliana na maradhi yaliyomuweka mbali na shughuli za umma kwa wiki kadhaa, akiwataka viongozi wa kisiasa kukumbatia mazungumzo na uvumilivu kwa ajili ya umoja wa kitaifa.

Oburu alitoa wito huo wakati wa mazungumzo na viongozi wa Bunge waliomtembelea nyumbani kwake jijini Nairobi, ambapo alikuwa akipata nafuu baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Seneta huyo alisema viongozi wana wajibu wa kuweka maslahi ya taifa mbele ya tofauti za kisiasa, akisisitiza kuwa mazungumzo ndiyo njia muhimu ya kuimarisha mshikamano na kuleta maendeleo.

Alisema Kenya inahitaji viongozi wanaoweza kujenga madaraja kati ya makundi yenye misimamo tofauti badala ya kuendeleza migawanyiko inayoweza kudhoofisha umoja wa wananchi.

Oburu alisisitiza kuwa uvumilivu wa kisiasa na kutafuta mwafaka ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za kitaifa, akiongeza kuwa viongozi wanapaswa kuwa tayari kusikilizana hata wanapokuwa na misimamo inayokinzana.

Kauli yake inajiri wakati ambapo viongozi wa kisiasa nchini wamekuwa wakikabiliana na tofauti za misimamo kuhusu masuala ya uongozi na mwelekeo wa taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Oburu alisema ugonjwa huo ulipunguza shughuli zake za kisiasa kwa muda, lakini akahakikisha wafuasi wake kuwa anaendelea kupata nafuu na atarejea katika ulingo wa siasa hivi karibuni.

“Ugonjwa ulipunguza shughuli zangu za kisiasa. Hivi karibuni nitarejea na kunguruma kwa namna ninayojua,” alisema.

Seneta huyo pia alieleza kuwa amekosa kushiriki mijadala ya Bunge na shughuli za kisiasa, akiwataka wafuasi wake kuendelea kumuombea na kuwa na subira anapoendelea kuimarika.

Wakati wa ziara hiyo, Oburu alidumisha ucheshi wake wa kawaida, akiwachekesha viongozi waliomtembelea licha ya changamoto za kiafya alizopitia.

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alisema viongozi hao walifurahishwa na maendeleo ya afya ya Oburu, lakini akamtaka kutanguliza afya yake na kutoharakisha kurejea katika shughuli za kisiasa kabla ya kupona kikamilifu.

Kwa upande wake, Spika wa Seneti Amason Kingi alisema Seneti imekosa mchango wa Oburu katika mijadala, shughuli za Bunge na masuala ya kitaifa, akitumai kuwa atarejea kazini baada ya kuimarika.

Oburu alishukuru viongozi hao kwa kumtembelea na kuonyesha mshikamano wakati wa kipindi chake cha kuugua, akiahidi kuendelea kuunga mkono umoja, amani na maendeleo ya Kenya.