Nchini Kenya,shule moja na maafisa waliohusika wameagizwa kulipa fidia ya Sh1.2 milioni baada ya Mahakama kupata kuwa haki ya mwanafunzi mmoja ya kulindwa kwa usiri wa taarifa zake za kiafya ilikiukwa kwa kufichuliwa kwa hali yake ya kuishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) bila ridhaa yake.
Mahakama ilibaini kuwa kufichuliwa kwa taarifa hizo kulimsababishia mwanafunzi huyo madhara ya kisaikolojia, unyanyapaa na kuvurugika kwa mahusiano yake na wanafunzi wenzake, baada ya taarifa za hali yake ya kiafya kusambaa katika mazingira ya shule na jamii.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, mwanafunzi huyo alikuwa akiishi na VVU tangu kuzaliwa, lakini aligundua hali yake mwaka 2018. Kupitia msaada wa mamake, alikuwa amejiunga na mpango wa kupata matibabu, ushauri nasaha na huduma nyingine za kiafya katika kituo cha Kangemi jijini Nairobi.
Mnamo Julai 2022, mfanyakazi wa taasisi iliyokuwa ikimhudumia alimwomba aandike simulizi ya maisha yake ili kuwasaidia na kuwatia moyo wasichana wengine waliojiunga na mpango huo.
Alihakikishiwa kuwa simulizi hilo lingetumiwa kwa madhumuni ya ushauri na ulezi wa wanafunzi wengine na kwamba taarifa zake zingebaki kuwa siri.
Hata hivyo, baadaye aligundua kuwa simulizi lake lilikuwa limechapishwa katika jarida la SkyGirls Magazine, huku jina lake kamili likionyeshwa mwishoni mwa makala hiyo.
Mwanafunzi huyo alisema uchapishaji huo ulimuweka katika hali ngumu baada ya marafiki zake, wanafunzi wenzake na baadhi ya watu katika jamii kugundua kuwa anaishi na VVU.
Rafiki yake wa zamani kutoka shule ya upili alithibitisha kuwa baada ya kusoma jarida hilo, aliwasiliana naye kutaka kujua ikiwa taarifa zilizochapishwa zilikuwa za kweli.
Shahidi mwingine aliyekuwa akisoma naye chuoni alieleza kuwa mwanafunzi huyo alianza kujitenga na kuonekana mwenye msongo wa mawazo, huku baadhi ya wanafunzi wakikataa kushirikiana naye katika shughuli za masomo.
Kwa upande wao, washtakiwa walidai kuwa mwanafunzi huyo alikuwa ametoa idhini ya simulizi lake kuchapishwa, lakini hawakuwasilisha ushahidi wa maandishi kuthibitisha madai hayo.
Katika uamuzi wake wa Februari 20, 2025, mwenyekiti wa mahakama hiyo, Carolyne Mboku, alisema kuandika simulizi la maisha hakumaanishi mtu ametoa idhini ya taarifa zake za kiafya kuchapishwa hadharani.
Mahakama iliamuru fidia ya Sh500,000 kwa kufichua hali yake ya kuishi na VVU bila ridhaa yake na Sh700,000 kwa madhara ya kisaikolojia, unyanyapaa na maumivu ya kihisia aliyopitia.
Aidha, wachapishaji waliamriwa kuondoa simulizi hilo kwenye tovuti yao ndani ya saa 24, huku taasisi zilizohusika zikitakiwa kuendesha mafunzo kwa wafanyakazi kuhusu usiri wa taarifa za kiafya.









