Rais William Ruto amefichua kuwa ukaguzi wa hivi karibuni wa sekta ya elimu nchini Kenya umebaini kuwepo kwa takriban wanafunzi 800,000 ambao majina yao yalikuwa kwenye sajili za shule za msingi licha ya kutokuwepo, huku shule karibu 200 zikibainika kuwepo kwenye karatasi pekee.
Matokeo hayo yanaibua maswali kuhusu usahihi wa takwimu zinazotumiwa na serikali katika kupanga na kugawa fedha za elimu, ikizingatiwa kuwa idadi ya wanafunzi waliosajiliwa ni mojawapo ya vigezo vinavyozingatiwa katika ufadhili wa shule.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa Pili wa Kitaifa kuhusu Elimu uliofanyika Naivasha, Kaunti ya Nakuru, Ruto alisema ukaguzi huo ulibaini kuwa takriban wanafunzi 87,000 katika shule za upili pia walikuwa wameorodheshwa kwenye sajili za serikali bila kuwepo.
Kwa mujibu wa Rais, hali hiyo imesababisha serikali kuendelea kutenga fedha za kugharamia wanafunzi ambao hawapo, huku baadhi ya taasisi za elimu zikinufaika na fedha za umma bila kuwa na shughuli zozote za masomo.
Ruto alisema kuwa serikali imekuwa ikipoteza kiasi kikubwa cha fedha kupitia mfumo wa kugawa fedha za uendeshaji wa shule, maarufu kama capitation, ambao hutegemea idadi ya wanafunzi waliosajiliwa katika kila taasisi.
Aidha, alifichua kuwa karibu shule 200 zilikuwa zimesajiliwa katika mifumo ya serikali lakini hazikuwepo katika hali halisi, jambo lililozua wasiwasi kuhusu namna usajili wa taasisi za elimu nchini unavyosimamiwa.
Rais alisema matokeo hayo yanaonyesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na uhakiki wa takwimu za elimu ili kuhakikisha fedha za umma zinawanufaisha wanafunzi na shule zilizopo.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, serikali imeelekeza Wizara ya Elimu kuharakisha uwekaji wa taarifa za wanafunzi na taasisi zote za elimu katika mifumo ya kidijitali ili kuboresha uwajibikaji na kuhakikisha takwimu zinazotumiwa katika kupanga bajeti ni sahihi.
Ruto pia alisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia kuziba mianya inayoweza kutumiwa na watu kujipatia fedha za umma kupitia udanganyifu wa takwimu za wanafunzi na shule.
Hatua hiyo inatarajiwa kusaidia kuboresha ugawaji wa rasilimali za elimu, ikiwemo fedha za uendeshaji, walimu, vitabu na vifaa vingine vya kujifunzia.
Wizara ya Elimu inatarajiwa kutumia mifumo hiyo kuimarisha ufuatiliaji wa wanafunzi kuanzia wanapojiunga na shule hadi wanapokamilisha safari yao ya masomo.
Matokeo hayo yanaongeza shinikizo kwa maafisa wa elimu na wasimamizi wa shule kuhakikisha kuwa taarifa wanazowasilisha serikalini zinaakisi hali halisi ya taasisi zao.









