Serikali ya Eswatini imezipa biashara zinazomilikiwa na raia wa kigeni na zinazofanya shughuli bila kufuata sheria za nchi hiyo kipindi cha miezi 12 kuondoka, katika hatua inayolenga kuimarisha usimamizi wa shughuli za kibiashara na kulinda nafasi za wajasiriamali wa ndani.
Hatua hiyo imeibua mjadala kuhusu nafasi ya wawekezaji wa kigeni katika uchumi wa nchi hiyo pamoja na namna serikali inavyokusudia kudhibiti biashara zinazokiuka masharti ya leseni na sheria za uwekezaji.
Mswada huo, unaojulikana kama Citizen Economic Empowerment Act, unalenga kuongeza ushiriki wa raia wa Eswatini, wanaojulikana kama emaSwati, katika shughuli za kiuchumi na kuwapa nafasi kubwa zaidi katika sekta ya biashara.
Hatua hiyo imefuatia malalamishi kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani ambao wamekuwa wakidai kuwa biashara zinazomilikiwa na wageni, hususan raia wa mataifa ya Asia, zimekuwa zikivamia maeneo ya biashara yaliyokuwa yakitawaliwa na wenyeji, na hivyo kuongeza ushindani unaotishia maisha yao ya kiuchumi.
Wabunge walifikia pendekezo hilo baada ya mjadala mkali kuhusu operesheni zinazoendeshwa na Wizara ya Biashara, Viwanda na Biashara dhidi ya maduka yanayomilikiwa na wageni, hasa katika maeneo ya vijijini yanayojulikana kama Swazi Nation Land.
Mbunge wa Mbabane Mashariki, Welcome Dlamini, alielezea wasiwasi wake kuhusu namna maafisa wa wizara hiyo walivyokuwa wakifunga maduka yanayomilikiwa na wafanyabiashara wa Asia bila kuwepo kwa mpango wa kuhakikisha wenyeji wanachukua nafasi zao.
Alisema baadhi ya maduka yamefungwa huku bidhaa zikiharibika na wafanyakazi ambao ni raia wa Eswatini wakipoteza ajira katika kipindi ambacho nchi hiyo tayari inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira.
Dlamini alipendekeza wafanyabiashara hao wapewe hadi miaka mitatu kuandaa mpito, akisema wenyeji wanahitaji muda wa kujifunza na kujiandaa kuendesha biashara hizo.
Hata hivyo, Mbunge wa Mafutseni, Sabelo Mtetwa, alipinga pendekezo la miaka mitatu akisema muda huo ni mrefu mno na unapunguza kasi ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Alipendekeza serikali badala yake ihakikishe wajasiriamali wa ndani wanapata ufadhili wa kutosha ili waweze kuchukua nafasi hizo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Nhlambeni, Manzi Zwane, aliunga mkono hoja ya kuwapa wageni muda zaidi, akionya kuwa kufungwa kwa biashara hizo ghafla kunaweza kuathiri ajira na upatikanaji wa bidhaa muhimu kwa wananchi.
Wakati huohuo, baadhi ya wabunge walionya dhidi ya kuwabagua wawekezaji wa kigeni kwa misingi ya uraia, wakisisitiza kuwa biashara zote zinazofuata sheria zinapaswa kuruhusiwa kuendelea na shughuli zake.
Wizara ya Biashara imesisitiza kuwa operesheni hizo hazilengi kufukuza wafanyabiashara wote wa kigeni, bali kuhakikisha kila biashara inafuata masharti ya leseni, sheria za uhamiaji na ulipaji kodi.
Eswatini, ambayo ni nchi isiyo na bahari kusini mwa Afrika na inapakana na Afrika Kusini na Msumbiji, inakabiliwa na changamoto za kiuchumi huku takribani asilimia 70 ya wananchi wake wakiishi chini ya kiwango cha umaskini.









