Waziri wa Afya Aden Duale ametangaza kupona na kuruhusiwa kuondoka hospitalini kwa mgonjwa wa mwisho wa Ebola aliyekuwa akipatiwa matibabu nchini, hatua inayotoa matumaini mapya katika juhudi za Kenya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo hatari.

Duale amesema hatua hiyo inafuatia kukamilika kwa matibabu ya mgonjwa huyo, huku watu 11 waliokuwa wakifuatiliwa kutokana na uwezekano wa kuwa wamekutana na wagonjwa wa Ebola nao wakiruhusiwa kutoka karantini baada ya kukamilisha muda wa uangalizi bila kuonyesha dalili za maambukizi.

Tangazo hilo linaashiria hatua muhimu katika vita vya Kenya dhidi ya Ebola, huku taifa likianza rasmi kuhesabu siku 42 zinazohitajika kabla ya kutangazwa kuwa limefanikiwa kuudhibiti mlipuko huo.

Kwa mujibu wa utaratibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), nchi inaweza kutangazwa kuwa haina Ebola baada ya kupita siku 42 tangu mgonjwa wa mwisho kuthibitishwa kupona au kufariki dunia, bila kuripotiwa kisa kingine kipya cha maambukizi.

Iwapo hakutakuwa na mgonjwa mwingine atakayethibitishwa kuwa na virusi vya Ebola katika kipindi hicho, Kenya inatarajiwa kutangazwa rasmi kuwa imeondokana na mlipuko huo ifikapo Disemba 23, 2026.

Hata hivyo, mamlaka za afya zinasisitiza kuwa kuondoka kwa mgonjwa wa mwisho hospitalini hakumaanishi kuwa hatari ya maambukizi imekwisha kabisa, bali ni mwanzo wa kipindi muhimu cha ufuatiliaji kinachohitaji tahadhari zaidi.

Wahudumu wa afya wanatarajiwa kuendelea kufuatilia hali ya wananchi ambao huenda walikutana na wagonjwa waliokuwa wameambukizwa, huku mifumo ya ufuatiliaji katika vituo vya afya ikiimarishwa ili kuhakikisha visa vyovyote vipya vinatambuliwa mapema.

Kenya imekuwa ikitekeleza hatua mbalimbali za kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo, ikiwemo kutambua watu waliokutana na wagonjwa, kuwafuatilia kiafya, kutoa huduma za matibabu na kuimarisha uchunguzi katika maeneo mbalimbali.

Mlipuko huo pia uliibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa kusambaa kwa virusi kupitia safari za ndani na kuvuka mipaka, hali iliyolazimu mamlaka za afya kuongeza umakini katika vituo vya kuingilia nchini.

Ebola ni ugonjwa hatari unaosababishwa na virusi na unaweza kusababisha homa kali, udhaifu wa mwili, maumivu ya misuli, kutapika na kuharisha, huku baadhi ya wagonjwa wakipata dalili kali za kutokwa na damu.

Ugonjwa huo huenea hasa kupitia kugusana moja kwa moja na damu au majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa, au vitu vilivyochafuliwa na majimaji hayo.

Wizara ya Afya inatarajiwa kuendelea kutoa taarifa kuhusu hali ya mlipuko huo kadri kipindi cha siku 42 kinavyoendelea, huku Wakenya wakisubiri kuona iwapo Disemba 23 itakuwa siku ya kihistoria ya kutangazwa rasmi kwa ushindi dhidi ya Ebola.