Mwanamke mmoja raia wa Kenya amehukumiwa adhabu ya kuchapwa viboko 100 nchini Saudi Arabia baada ya kupatikana na hatia ya kupata ujauzito nje ya ndoa, katika kesi inayoibua maswali kuhusu usalama na haki za wafanyakazi wa Kenya wanaoishi na kufanya kazi katika mataifa ya Mashariki ya Kati.
Mwanamke huyo ametambuliwa kama Esther Wanja Muthoni, mwenye umri wa miaka 40 na mama wa watoto watano, ambaye amekuwa akifanya kazi nchini Saudi Arabia kama mfanyakazi wa nyumbani kupitia kampuni ya uajiri ya Maharah Human Resources.
Kwa mujibu wa taarifa kuhusu kesi hiyo, Muthoni alipata ujauzito kufuatia uhusiano wa muda mfupi na mwanamume raia wa Misri aliyekuwa akiishi Saudi Arabia.
Mwanamume huyo baadaye aliondoka nchini humo na kumuacha Muthoni akilea mtoto wao bila msaada wake.
Muthoni alijifungua mtoto wa kiume, Abudy, mwezi Agosti 2025 katika makazi ya wafanyakazi.
Hata hivyo, baada ya msimamizi wa makazi kumfahamu mama huyo na mtoto wake, walipelekwa hospitalini ambako maafisa wa polisi walimkamata kwa mahojiano kuhusu ujauzito huo.
Baadaye alikabiliwa na mashtaka ya kufanya mapenzi nje ya ndoa, kosa linalochukuliwa kuwa la jinai chini ya tafsiri ya sheria za Kiislamu zinazotumika nchini Saudi Arabia.
Kesi yake ilisikilizwa na jopo la majaji watatu katika mahakama ya jinai jijini Riyadh, huku vikao kadhaa vikiendelea katika kipindi cha kiangazi kabla ya hukumu kutolewa Oktoba 2026.
Taarifa zinaeleza kuwa Muthoni alikuwa na mkalimani wa mahakama lakini hakuwa na wakili wa kumwakilisha katika kesi hiyo.
Changamoto zake hazikuishia hapo kwani baada ya kuachiliwa kutoka kizuizini, alikosa makazi baada ya kunyimwa nafasi ya kurejea katika makazi ya wafanyakazi na pia kukosa msaada katika kituo cha hifadhi.
Hali hiyo ilimlazimu kuishi kwa muda katika kituo cha mafuta jijini Riyadh ambako wanawake wengine wahamiaji waliokuwa wakijaribu kurejea mataifa yao pia walikuwa wamekusanyika.
Baadaye mwajiri wake alimpatia makazi, huku Ubalozi wa Kenya nchini Saudi Arabia ukimpatia hati za kusafiria ili aweze kurejea nyumbani pamoja na mwanawe.
Hata hivyo, kesi iliyokuwa ikiendelea ilimzuia kuondoka, na hati hizo zimepitwa na wakati.
Muthoni hakukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo akisema kipaumbele chake ni kurejea Kenya na kuungana na watoto wake wengine wanne.
Bado haijabainika ni lini adhabu hiyo itatekelezwa au iwapo kifungo cha mwaka mmoja cha kufukuzwa eneo husika kitamwezesha kurejea Kenya.
Hukumu hiyo imeibua upya mjadala kuhusu ulinzi wa wafanyakazi wa Kenya wanaoishi na kufanya kazi katika mataifa ya Mashariki ya Kati.









