Serikali ya Marekani imewafungulia mashtaka watu sita wanaohusishwa na shughuli za uhalifu barani Afrika, wanaotuhumiwa kushiriki katika mpango wa utapeli wa uwekezaji wa sarafu za kidijitali uliodaiwa kuwalaghai mamia ya raia wa Marekani.
Washukiwa hao wanadaiwa kutumia majukwaa bandia ya uwekezaji wa ankara zisizoweza kubadilishwa, maarufu kama Non-Fungible Tokens (NFTs), kuwashawishi waathiriwa kuwekeza fedha zao kabla ya kuzihamisha kupitia mifumo ya miamala ya sarafu za kidijitali.
Mashtaka hayo yalitangazwa na mwanasheria wa Marekani mjini Columbia, Jeanine Ferris Pirro, alisema kesi hiyo ni sehemu ya juhudi pana za kupambana na mitandao ya uhalifu wa kimataifa inayotumia mahusiano ya mtandaoni na sarafu za kidijitali kuwaibia watu.
Kwa mujibu wa Wizara ya Sheria ya Marekani, washukiwa hao wanadaiwa kuwa na uhusiano na watu kutoka Kusini-Mashariki mwa Asia na China, huku shughuli zao zikidaiwa kuendeshwa katika vituo vya utapeli nchini Madagascar kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2025.
Wachunguzi wanashuku kuwa shughuli hizo huenda zilihamishiwa Madagascar kutoka Cambodia baada ya mamlaka za usalama kuimarisha operesheni dhidi ya mitandao ya utapeli nchini humo.
Katika mpango huo, washukiwa wanadaiwa kujifanya wanawake wenye kuvutia kwenye tovuti za kutafuta wapenzi na mitandao ya kijamii ili kuanzisha mahusiano na Wamarekani.
Baada ya kujenga uaminifu kwa waathiriwa, washukiwa hao wanadaiwa kuwashawishi kuwekeza katika majukwaa bandia ya NFT kwa kuunganisha pochi zao za sarafu za kidijitali na tovuti hizo.
Waathiriwa walishawishiwa kuweka fedha zaidi baada ya kuunganishwa kwa pochi hizo, lakini fedha hizo zimedaiwa kuchukuliwa bila wao kujua kuwa walikuwa wakishiriki katika mpango wa ulaghai.
Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) ulibaini takribani pochi 74 za sarafu za kidijitali zilizohusishwa na waathiriwa wapatao 800 katika maeneo mbalimbali nchini Marekani.
Waathiriwa hao waliripoti kupata hasara za kifedha baada ya kuingiliana na majukwaa hayo ya uwekezaji yaliyodaiwa kuwa ya udanganyifu.
Wachunguzi wanasema fedha zilizoibwa zilihamishwa hadi kwenye akaunti za sarafu za kidijitali zinazohusishwa na watu walioko China.
Miongoni mwa wanaokabiliwa na mashtaka ni Chui Kok Wa, anayetuhumiwa kuwa kiongozi wa mpango huo wa ulaghai wa uwekezaji wa NFT.
Anakabiliwa na shtaka la kula njama ya kutekeleza ulaghai kupitia mawasiliano ya kielektroniki.
Nyaraka za mahakama zinaonyesha kuwa wachunguzi walipata simu zilizokuwa na mikataba ya ajira, ratiba za kazi na maandishi yaliyotumiwa kuwaelekeza wafanyakazi namna ya kuwadanganya waathiriwa.
Maelekezo hayo yanadaiwa kueleza jinsi wafanyakazi walivyopaswa kutumia hisia na mahusiano ya kimapenzi kuwashawishi watu kuwekeza fedha zao.
Aidha, wachunguzi walipata rekodi zilizokuwa na taarifa binafsi za wafanyakazi, mishahara yao, saa za kazi na anwani za pochi za sarafu za kidijitali.
Kesi hiyo inaangazia namna mitandao ya uhalifu inavyotumia mahusiano ya kimapenzi na majukwaa ya uwekezaji mtandaoni kuwavutia waathiriwa, kabla ya kuwatapeli fedha zao kwa kutumia teknolojia ya sarafu za kidijitali.









