Nairobi:Mshukiwa Wa Kujifanya Polisi Akamatwa Embakasi

Katika kuelekea msimu wa likizo ya Desemba, matukio ya uhalifu yanaweza kuongezeka huku watu wengi wakifanya safari na shughuli mbalimbali za kifedha.

Kufuatia hali hiyo, polisi jijini Nairobi na maeneo mengine nchini wanaendesha misako maalum kukabiliana na wahalifu wanaolenga wananchi, hususan wale wanaotoa fedha katika kwenye taasisi husika.

Katika operesheni hiyo, maafisa wa upelelezi wamemkamata mshukiwa anayedaiwa kuhusika na msururu wa matukio ya ujambazi ambapo wahalifu huwalenga watu muda mfupi baada ya kutoa fedha benki.

Mshukiwa huyo alikamatwa katika eneo la Embakasi Village, Nairobi, kufuatia uchunguzi wa kina uliofanywa na maafisa kutoka kikosi cha Operation Action Team (OAT) na Kitengo cha Utafiti wa Uhalifu na Ujasusi (CRIB).

Kwa mujibu wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), washukiwa hao hutumia mbinu ya kujifanya maafisa wa trafiki ili kuwazuia na kuwaibia wananchi wanaotoka benki wakiwa na fedha.

Wahalifu hao wanadaiwa kutumia mwonekano na mamlaka yanayohusishwa na sare za polisi kuwafanya waathiriwa wasiwe na mashaka kabla ya kuwavamia na kuwaibia.

Kupitia ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia na uchunguzi wa kitaalamu wa vielelezo, wapelelezi waliwatambua washukiwa wanne wanaoaminika kuhusishwa na matukio hayo.

Miongoni mwao ni Muia Mutune, anayejulikana pia kwa jina la Fredrick Mbuta, ambaye alikamatwa Aprili 2026 kuhusiana na visa kama hivyo kabla ya kuachiliwa kwa dhamana Julai mwaka huo.

Wapelelezi waliendeleza uchunguzi na kufuatilia taarifa zilizowaelekeza hadi Embakasi Village, ambako mshukiwa huyo alikamatwa.

Kwa sasa, anazuiliwa na polisi huku taratibu za kumfikisha mahakamani zikiendelea.

Wakati huohuo, maafisa wa upelelezi wameendeleza juhudi za kuwatafuta washukiwa wengine wanaodaiwa kuhusika na mtandao huo wa uhalifu, ambao bado hawajakamatwa.

DCI imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia wahalifu wanaohusika na vitendo vya ukatili na ujambazi ili kuhakikisha usalama wa wananchi.

Wananchi wametakiwa kuwa waangalifu wanaposhughulikia fedha taslimu, hasa wanapotoka benki, na kuripoti kwa polisi vitendo vyovyote vinavyotia shaka.

Hata hivyo,baada ya kukamatwa washukiwa husubiri taratibu kabla ya kuandaliwa jalada la kufikishwa mahakamani.