Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo), Félix Tshisekedi, amemtuhumu mtangulizi wake Joseph Kabila kwa kufanya kazi kwa niaba ya Rwanda katika mzozo wa kivita unaoendelea katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Tshisekedi alitoa tuhuma hizo alipohutubia wabunge wanaomuunga mkono, akidai kuwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, amemsukuma Kabila kujiunga na mapigano yanayolenga serikali yake.
Akizungumza katika hotuba iliyorushwa kupitia mtandao wa kijamii wa X na urais wa Congo Jumanne, Oktoba 27, 2026, Tshisekedi alidai kuwa kurejea kwa Kabila katika ulingo wa kisiasa na kijeshi kunahusishwa na juhudi za Rwanda kuongeza ushawishi wake katika mashariki mwa Congo.
Rais huyo alidai kuwa hatua ya Kabila kujitokeza tena na kuchukua nafasi katika uasi huo inaonyesha kuwa wapinzani wake wanakabiliwa na changamoto katika kutekeleza malengo yao.
Tuhuma hizo zinajiri baada ya Kabila kujiunga na vuguvugu la waasi la M23, linaloungwa mkono na Rwanda, na kuhusika moja kwa moja katika uasi unaoendelea katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini.
Kabila anatarajiwa kuongoza muungano mpya unaojulikana kama Front for the Refoundation of the Nation (FRN), huku viongozi wa M23 wakitarajiwa kushikilia nyadhifa za naibu viongozi.
Muungano huo umetangaza nia ya kuunganisha nguvu na rasilimali zake ili kuikabili serikali ya Kinshasa, ukidai kuwa unalenga kukomesha kile unachokitaja kuwa utawala wa kidhalimu.
Kabila aliongoza DR Congo kati ya mwaka 2001 na 2019. Mwaka uliopita, alihukumiwa kifo akiwa hayupo mahakamani baada ya mamlaka za Congo kumhusisha na uhaini na kushirikiana na waasi wa M23.
Hata hivyo, amekanusha tuhuma zinazomhusisha na uasi huo.
Mapigano mashariki mwa Congo yameendelea licha ya juhudi za kidiplomasia za kutafuta suluhu. M23 imechukua maeneo kadhaa muhimu, yakiwemo miji ya Goma na Bukavu, huku hali ya usalama ikiendelea kuwa tete.
Wakati huohuo, upinzani wa Congo umekataa kuunga mkono kunyakuliwa kwa mamlaka kwa nguvu, ukitaka mazungumzo jumuishi yatakayohusisha pande zote zinazohusika katika mzozo huo.
Mvutano huo unaendelea huku Tshisekedi akikabiliwa na ukosoaji kuhusu uwezekano wa mabadiliko ya katiba yatakayomruhusu kuwania muhula wa tatu baada ya muhula wake wa sasa kukamilika mwaka 2028.









