Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) imewakamata madereva na kuzuilia magari 13 kufuatia operesheni ya ukaguzi wa usalama.
Oparesheni hiyo imefanywa katika barabara ya Southern Bypass jijini Nairobi, huku mamlaka hiyo ikiimarisha juhudi za kukabiliana na ajali za barabarani nchini.
Operesheni hiyo ilifanywa usiku wa Jumatano na Alhamisi, Oktoba 28 na 29, 2026, na kikosi cha pamoja cha maafisa kutoka idara mbalimbali za serikali, kwa lengo la kuhakikisha madereva na magari yanazingatia sheria za trafiki.
Kwa mujibu wa NTSA, ukaguzi huo ulibaini ukiukaji kadhaa wa sheria za barabarani, ukiwemo baadhi ya madereva kuendesha magari wakiwa wamelewa na wengine kutumia leseni za udereva zilizokwisha muda wake.
Mamlaka hiyo pia ilibaini magari yaliyokuwa yakiendeshwa bila bima halali, huku mengine yakikiuka masharti yaliyowekwa katika bima zao.
Aidha, baadhi ya magari yaliyokaguliwa yalikuwa na vyeti vya ukaguzi wa magari vilivyokwisha muda wake, hali inayozua wasiwasi kuhusu uzingatiaji wa viwango vya usalama vinavyohitajika kabla ya magari kuruhusiwa kuendelea kutumia barabara za umma.
Kasoro nyingine zilizobainika ni pamoja na magari yaliyokuwa na taa za mbele zilizoharibika pamoja na vioo vya mbele vilivyopasuka, ambavyo vinaweza kuhatarisha usalama wa madereva na watumiaji wengine wa barabara, hasa nyakati za usiku.
Operesheni hiyo inajiri siku chache baada ya NTSA kutangaza kampeni ya Msimu Bila Ajali, Usalama Barabarani, inayolenga kupunguza ajali na vifo vinavyotokana na uzembe na ukiukaji wa sheria za trafiki.
Kupitia kampeni hiyo, mamlaka hiyo imesema itaendesha ukaguzi wa mchana na usiku katika barabara kuu zinazotumiwa na magari mengi, huku madereva na abiria wakielimishwa kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama.
Ukaguzi huo unajumuisha pia kuhakikisha magari ya uchukuzi wa umma yana vifaa vya kudhibiti mwendo vinavyofanya kazi, leseni zinazotambulika na nyaraka zinazohitajika kisheria.
NTSA imewataka madereva kupunguza mwendo, kudumisha umbali salama kati ya magari na kuhakikisha wanazingatia sheria zote za barabarani.
Mamlaka hiyo pia imesisitiza umuhimu wa kufunga mikanda ya usalama katika safari zote na kuepuka kuendesha gari baada ya kutumia vileo, ikionya kuwa hatua hizo zinaweza kusaidia kuzuia ajali na kuokoa maisha.
Aidha, madereva wametakiwa kuhakikisha magari yao yako katika hali nzuri kabla ya kuanza safari yoyote.









