Zaidi ya shule 300 nchini Italia zimehamisha wanafunzi na wafanyakazi baada ya kupokea ujumbe mmoja wa vitisho vya kuwepo kwa mabomu, katika tukio lililoibua taharuki na kuanzisha uchunguzi wa kiusalama.

Waziri wa Elimu nchini Italia, Giuseppe Valditara, amesema shule hizo zilipokea ujumbe unaofanana wa tahadhari ya bomu, na kusababisha mamlaka kuchukua hatua za haraka za kuwahamisha waliokuwa ndani ya majengo hayo.

Valditara amesema huenda vitisho hivyo vilikuwa vya uongo, akiongeza kuwa idadi ya shule zilizoathiriwa inaweza kuongezeka. Waziri huyo amesisitiza kuwa hakuna haja ya kuzua hofu isiyo ya lazima, huku mamlaka zikichunguza chanzo cha ujumbe huo.

Barua pepe iliyotumwa kwa shule hizo ilidai kuwa kifaa chenye vilipuzi na mfumo wa kukilipua kwa mbali kilikuwa kimewekwa ndani ya majengo.

Ujumbe huo ulisainiwa kwa jina la “Mikhail Andropov, kiongozi wa Vilayat of Misoginistan”, kulingana na nakala ya barua hiyo iliyoonekana na Reuters.

Mtu huyo huyo anayedaiwa kuwa mtumaji pia alihusishwa na vitisho vya barua pepe vilivyotumwa kwa vyumba vya habari nchini Ireland na Bulgaria siku ya Ijumaa iliyopita.

Polisi nchini Italia wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha ujumbe huo na wahusika wake, huku maeneo yaliyoathiriwa yakikaguliwa kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine.

Tukio hilo limeibuka wakati mataifa mbalimbali ya Ulaya yakikabiliwa na ongezeko la vitisho vya kiusalama na mashambulizi ya kimtandao yanayolenga kuvuruga huduma muhimu.

Shule nchini Scotland, Ireland Kaskazini na Jamhuri ya Ireland pia ziliripoti kupokea barua pepe zenye vitisho vinavyofanana.

Hata hivyo, mamlaka nchini Scotland na Ireland Kaskazini zilisema vitisho hivyo havikuchukuliwa kuwa vya kuaminika, hivyo shule nyingi ziliendelea na shughuli za kawaida bila kuhamishwa wanafunzi.

Matukio hayo yanajiri kufuatia visa vingine vya vitisho na mashambulizi ya kimtandao vilivyolenga maduka makubwa, benki za damu, mifumo ya usafiri wa anga na vituo vya televisheni barani Ulaya.

Baadhi ya viongozi wa Ulaya wameeleza wasiwasi kuwa huenda matukio hayo yakawa sehemu ya mikakati ya kuvuruga utulivu na kueneza hofu katika mataifa yanayounga mkono Ukraine.

Hata hivyo, hakuna uthibitisho uliotolewa hadharani kuhusu nani hasa aliyehusika na vitisho vya shule nchini Italia.

Serikali ya Italia na vyombo vya usalama vinaendelea kufuatilia hali hiyo huku uchunguzi ukiendelea.