Hisa za kampuni ya teknolojia ya Nvidia zilishuka kwa kasi katika biashara ya baada ya saa za kawaida za soko Jumatano, kufuatia ripoti kwamba Mkurugenzi Mkuu wake Jensen Huang alikuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa na afisa mkuu wa kampuni hiyo.

Kushuka kwa hisa hizo kulitokea huku bodi ya kampuni hiyo ikiripotiwa kufanya mkutano kujadili hatma ya Huang, ambaye amekuwa akiongoza kampuni hiyo kwa miaka 33 tangu ilipoanzishwa.

Kwa mujibu wa CNN, ripoti ya gazeti la The New York Times ilidai kuwa Huang alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na afisa wa kampuni hiyo anayemripoti moja kwa moja.

Hali hiyo ilizidisha mgogoro unaoikumba Nvidia, ambayo tayari ilikuwa ikikabiliwa na uchunguzi kuhusu madai ya uhusiano wa Huang na mwanamke anayeshukiwa na maafisa wa Marekani kuwa jasusi wa China.

Gazeti la Wall Street Journal pia liliripoti kuwa bodi ya Nvidia ilikuwa ikijiandaa kumuondoa Huang madarakani, jambo lililozua wasiwasi miongoni mwa wawekezaji kuhusu mustakabali wa kampuni hiyo.

Hisa za Nvidia zilishuka kwa zaidi ya asilimia tisa katika biashara ya baada ya saa za kawaida za soko, kabla ya kupunguza baadhi ya hasara na kufikia kushuka kwa takriban asilimia 7.2 kufikia saa saba usiku kwa saa za Marekani.

Kampuni hiyo haikuwa imetoa majibu rasmi kuhusu ripoti mpya za uhusiano wa Huang na mkutano wa bodi kufikia wakati habari hiyo ilipochapishwa.

Huang, ambaye ni mwanzilishi mwenza wa Nvidia, alikiri Jumapili kuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa na kuomba radhi, bila kutaja mtu mwingine aliyehusika.

Bodi ya kampuni hiyo pia ilitangaza uchunguzi kuhusu madai kwamba Huang alikuwa mlengwa wa operesheni ya kijasusi ya kigeni.

Mkurugenzi huyo amekuwa mtu muhimu katika ukuaji wa Nvidia, ambayo imekuwa mojawapo ya kampuni zenye thamani kubwa duniani kutokana na kuongezeka kwa teknolojia ya akili mnemba (AI).

Vifaa zinazotengenezwa na Nvidia hutumiwa kuendesha mifumo mbalimbali ya AI, ikiwemo ChatGPT ya OpenAI na Claude ya Anthropic.

Kutokuwa na mrithi wa wazi wa Huang kumeongeza wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuondoka kwake, huku wawekezaji wakitathmini athari zinazoweza kujitokeza kwa kampuni hiyo na sekta nzima ya teknolojia.

Kushuka kwa hisa za Nvidia pia kumeathiri masoko mapana ya Marekani, huku mikataba ya baadaye ya Nasdaq 100 na S&P 500 ikishuka.

Wakati huo huo, hisa za kampuni pinzani za kutengeneza chips, Advanced Micro Devices (AMD) na Broadcom, zilipanda katika biashara ya baada ya saa za kawaida za soko.