Wabunge kadhaa waliohama chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto na kujiunga na chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, wamepoteza nyadhifa muhimu katika kamati mbalimbali za Bunge la Taifa kufuatia mabadiliko mapya ya uongozi wa kamati hizo.
Mabadiliko hayo yaliyoidhinishwa wakati wa kikao cha Jumanne jioni katika majengo ya Bunge yaliwaathiri Mbunge wa Gilgil Martha Wangari, Mbunge wa Gatundu Kusini Gabriel Kagombe na Mwakilishi wa Wanawake wa Nyeri Rahab Mukami, ambao waliondolewa katika baadhi ya nyadhifa walizokuwa wakishikilia.
Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga, aliyehama chama cha Ford Kenya na kujiunga na vuguvugu la Linda Mwananchi linalohusishwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, pia ameathirika na mabadiliko hayo.
Wangari amepoteza nafasi yake katika jopo la wenyeviti wa Bunge (Speaker's Panel), ambako alikuwa Mwenyekiti wa Kwanza, pamoja na uanachama wake katika Kamati ya Ulinzi, Ujasusi na Mahusiano ya Kigeni.
Nafasi yake katika kamati hiyo imechukuliwa na Mbunge wa Njoro Charity Kathambi, huku Wangari akihamishiwa katika Kamati ya Masuala ya Diaspora na Wafanyakazi Wahamiaji.
Kwa upande wake, Kagombe ameondolewa katika Kamati ya Kilimo na Mifugo ambako nafasi yake imechukuliwa na Mbunge wa Gatundu Kusini Elijah Kururia.
Pia amepoteza nafasi katika Kamati ya Hesabu za Umma (PAC), ambayo sasa itawakilishwa na Mbunge wa Maragua Mary Wamaua. Hata hivyo, Kagombe amepewa nafasi katika Kamati ya Usimamizi wa Utekelezaji wa Katiba.
Mukami naye ameondolewa katika Kamati ya Leba, huku nafasi yake ikichukuliwa na Mbunge wa Juja George Koimburi. Baadaye aliteuliwa kujiunga na Kamati ya Ushirikiano wa Kikanda.
Aidha, Mukami amepoteza nafasi yake katika ujumbe wa Kenya kwenye Bunge la Afrika (Pan-African Parliament), ambayo sasa itashikiliwa na Wamaua.
Kalasinga naye ameondolewa katika Kamati ya Hesabu za Mifuko Maalum, huku nafasi yake katika Bunge la Afrika ikichukuliwa na Mbunge wa Mount Elgon Fred Kapondi.
Akitetea mabadiliko hayo, Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung'wah alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha uwakilishi wa Kenya katika Bunge la Afrika na kuwapa wabunge wengine nafasi ya kupata uzoefu wa shughuli za kikanda.
Hata hivyo, Ichung'wah alidokeza kuwepo kwa malalamishi kuhusu utendaji wa baadhi ya wawakilishi waliokuwa wakihudumu katika taasisi hiyo, akisema walikuwa wameibua wasiwasi kwa uongozi wa Bunge.
Alisema Kenya inahitaji wawakilishi wanaoweza kueleza misimamo ya taifa kwa ufasaha katika mikutano ya kimataifa bila kuiaibisha nchi.
Naibu Kiongozi wa Wengi Owen Baya aliunga mkono mabadiliko hayo, akisema ujumbe wa Kenya uliwahi kushindwa kuchangia ipasavyo mjadala kuhusu uraia na utaifa katika mkutano wa Bunge la Afrika.
Mabadiliko hayo pia yalihusisha kamati nyingine za Bunge, huku wabunge kadhaa wakihamishwa katika nyadhifa tofauti.
Ingawa hoja zilizowasilishwa hazikuhusisha moja kwa moja mabadiliko hayo na kuhama kwa wabunge kisiasa, hatua hiyo imezua mjadala kuhusu nafasi ya misimamo ya kisiasa katika ugawaji wa nyadhifa za Bunge kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.









