Kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, amempa Seneta wa Nyandarua John Methu jukumu la kuongoza mikakati ya kukijenga chama hicho katika maeneo mbalimbali nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Katika mabadiliko hayo ya majukumu ndani ya chama hicho cha upinzani, Methu atakuwa akisimamia ufunguzi rasmi wa ofisi za DCP kote nchini pamoja na kuratibu shughuli za kuwahamasisha wafuasi na kuimarisha ushawishi wa chama katika ngazi za mashinani.

Gachagua amesema hatua hiyo itamwezesha yeye kujikita katika maandalizi ya uchaguzi wa mchujo wa chama hicho, utakaowezesha kupata wagombeaji watakaokiwakilisha katika uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza Jumanne, Novemba 24, Gachagua alisema amempokea Methu kurejea katika majukumu yake baada ya mapumziko ya wiki mbili na kumweleza kuhusu mipango na shughuli zinazotarajiwa kutekelezwa na chama hicho.

"Kuanzia sasa, Katibu Mkuu mteule ataongoza timu katika kufungua rasmi ofisi zote za chama cha DCP na kuendesha shughuli za uhamasishaji wa kisiasa katika ngazi za mashinani, hatua itakayonipa nafasi ya kujikita katika maandalizi ya uchaguzi wa mchujo wa chama," alisema Gachagua.

Methu, ambaye ni Katibu Mkuu mteule wa DCP, amekuwa mmoja wa viongozi wanaoshiriki katika shughuli za kisiasa za chama hicho, hasa katika juhudi za kukipanua na kukijengea miundo ya uongozi katika maeneo mbalimbali.

Gachagua pia ametangaza kuwa viongozi wa chama hicho hawatakuwa na mapumziko ya kawaida ya sikukuu za Krismasi mwaka huu, akisema watakuwa na siku mbili pekee za mapumziko, Desemba 25 na 26.

Amesema yeye, Methu na timu yao wataendelea na shughuli za kisiasa katika kipindi chote cha sikukuu, akitaja umuhimu wa maandalizi ya uchaguzi wa 2027 kuwa sababu ya kutopumzika kwa muda mrefu.

"Seneta Methu, mimi na timu yetu hatutakuwa na muda wa mapumziko ya Krismasi isipokuwa Desemba 25 na 26. Kazi iliyoko mbele yetu ya kuikomboa nchi kutoka kwa mawakala wa ufisadi na kutoheshimu utawala wa sheria haitupi nafasi ya anasa," alisema.

Gachagua pia amezitaka familia za viongozi wa chama hicho kuwaelewa kutokana na ratiba yao yenye shughuli nyingi katika kipindi cha sikukuu, akiahidi kuwa watapata fursa ya kusherehekea pamoja baada ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Alisema wanatarajia kufidia muda watakaokosa kuwa na familia zao wakati wa Krismasi mwaka huu kwa kusherehekea pamoja Desemba 2027.

Hatua ya kumkabidhi Methu jukumu la kuratibu shughuli za mashinani inajiri wakati DCP ikiendelea kupanua ushawishi wake kisiasa na kuvutia viongozi kutoka vyama vingine kuelekea uchaguzi mkuu ujao.