Hatima ya kiwanda cha kusaga na kusindika mchele cha Mwea Rice Mills Limited inatarajiwa kujulikana Januari 20, 2027, wakati Mahakama Kuu mjini Kerugoya itakapotoa uamuzi kuhusu kesi inayopinga mipango ya serikali kukibinafsisha.

Jaji Joyce Gandani ndiye aliyepanga tarehe hiyo ya kutolewa kwa hukumu jana baada ya pande zote katika kesi hiyo kuwasilisha hoja zao za mwisho mahakamani.

Kesi hiyo ilifunguliwa mwaka 2023 na wakulima wawili wa mpunga kutoka Mwea, John Munene Jecinta na Pius Njogu Kathuri, baada ya serikali kukijumuisha kiwanda hicho katika mpango wa kubinafsisha mashirika 11 yanayomilikiwa na serikali.

Wakulima hao, ambao ni wanachama wa Mwea Rice Growers Multipurpose Co-operative Society Limited, wanawakilishwa na wakili Kahiga Kiguru.

Wanapinga hatua ya serikali wakisema kuwa uamuzi wa kubinafsisha kiwanda hicho ulifanywa bila kuwapa wakulima na wadau wengine fursa ya kutosha kushiriki katika mchakato wa mashauriano ya umma.

Kwa mujibu wa walalamishi hao, serikali ilipanga mkutano wa mashauriano ya umma katika Chuo cha Polytechnic cha Nyeri, Kaunti ya Nyeri, Desemba 11, 2023, badala ya kuufanyia katika Kaunti ya Kirinyaga ambako wakulima wengi wa mpunga wa Mwea wanaishi na kufanya shughuli zao za kilimo.

Walisema kuwa muda wa saa nne uliotengwa kwa mkutano huo usingewapa maelfu ya wakulima nafasi ya kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.

Wakulima hao wanasisitiza kuwa mashauriano hayo hayakuwa na maana iwapo sehemu kubwa ya watu ambao wangeathiriwa moja kwa moja na uamuzi huo hawakuweza kushiriki ipasavyo.

Katika ombi lao la dharura, walalamishi walidai kuwa miongozo, mfumo na vigezo vilivyotumika kuamua kubinafsisha kiwanda hicho vilikiuka Katiba ya Kenya, hasa masharti yanayohusu ushiriki wa umma, usawa, upatikanaji wa taarifa na ulinzi wa haki za mali.

Walitaja Ibara za 10(2), 27, 35, 40, 47(1)(2) na 96 za Katiba, wakitaka mahakama iingilie kati kuzuia utekelezaji wa mpango huo hadi kesi yao itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Desemba 1, 2023, Jaji R. Mwongo aliidhinisha ombi hilo kama la dharura na kutoa maelekezo kuhusu namna ya kuwasilisha nyaraka za kesi hiyo kwa wahusika na muda wa kuwasilisha majibu yao.

Serikali inataka kubinafsisha Mwea Rice Mills Limited kama sehemu ya mpango wake wa kupunguza mzigo wa kifedha unaotokana na kuendesha mashirika ya umma.

Serikali imesema kuwa kuhusisha wawekezaji wa kibinafsi kunaweza kusaidia kuleta mitambo ya kisasa, mtaji na ufanisi katika shughuli za kiwanda hicho ili kukifanya kiwe na uwezo mkubwa wa kujiendesha kibiashara.

Hata hivyo, wakulima wanaopinga hatua hiyo wanasema kuwa mustakabali wa kiwanda hicho una umuhimu mkubwa kwa maelfu ya watu wanaotegemea kilimo cha mpunga katika eneo la Mwea.

Serikali inamiliki asilimia 55 ya hisa za kiwanda hicho kupitia Mamlaka ya Kitaifa ya Umwagiliaji (NIA), huku wakulima wakimiliki asilimia 45 kupitia chama chao cha ushirika.

Wakulima hao wanasema kuwa umiliki wao wa hisa unawapa sababu ya msingi ya kutaka kusikilizwa kabla ya uamuzi wowote unaoweza kubadilisha umiliki na usimamizi wa kiwanda hicho kufanywa.

Akizungumza baada ya kutangazwa kwa tarehe ya hukumu, mkulima Nathan Kariuki alisema wakulima wote katika Skimu ya Umwagiliaji ya Mwea wanatazamia kwa hamu uamuzi wa mahakama.

Wakulima watahudhuria mahakamani Januari 20, 2027, ili kufahamu hatima ya kiwanda hicho ambacho wanamiliki sehemu ya hisa.

"Tutakuwa hapa siku hiyo kusikia iwapo kiwanda kitabinfsishwa, kwa sababu tuna hisa zetu za asilimia 45," alisema Kariuki.

Wakulima hao pia walitaja changamoto mbalimbali zinazowakabili katika skimu hiyo, zikiwemo ndege aina ya kwelea wanaoharibu mpunga, uvamizi wa konokono, uingizaji wa mchele kutoka nje kabla ya mchele wa Mwea kuuzwa sokoni na hali mbaya ya barabara za mashambani.

Kariuki alisema kuwa wakulima wanahitaji pia hatua zichukuliwe kushughulikia matatizo hayo yanayoathiri uzalishaji na maisha yao.

Aliongeza kuwa angependa wakulima hao, kupitia viongozi wao katika kesi hiyo, wafungue kesi nyingine kupinga Mamlaka ya Kitaifa ya Umwagiliaji kukusanya fedha kutoka kwa wakulima kupitia mfumo wa eCitizen kwa ajili ya huduma za maji.

Kwa maoni yake, fedha hizo zinaweza kusaidia katika matengenezo ya barabara za mashambani ambazo ziko katika hali mbaya.

Naye Mary Wagatwe, mkazi wa sehemu ya Thiba, alilalamikia viongozi waliochaguliwa akisema kuwa hawajazingatia ipasavyo changamoto zinazowakabili wakulima.

Alisema kuwa badala ya viongozi hao kushughulikia matatizo ya wananchi, wamekuwa wakitumia muda mwingi katika mizozo ya kisiasa.

Wakulima hao sasa wanasubiri uamuzi wa mahakama, wakitumaini kuwa utatoa mwelekeo kuhusu mustakabali wa kiwanda hicho na nafasi yao kama wanahisa.