Baadhi ya viongozi wanaounga mkono serikali ya Rais William Ruto wamewakashifu viongozi wa upinzani kwa matamshi yao dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), wakidai wanaiingilia taasisi hiyo huru katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Viongozi hao wamewataka wanasiasa kuheshimu uhuru wa IEBC na kuipa nafasi ya kutekeleza majukumu yake bila shinikizo la kisiasa, wakieleza kuwa maandalizi ya uchaguzi yanapaswa kuachwa mikononi mwa taasisi husika kwa mujibu wa sheria.
Wakizungumza katika mkutano wa kisiasa, viongozi hao pia walielekeza mashambulizi yao kwa kinara wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, wakimtuhumu kwa kuendeleza siasa za kikabila na kudai kuwa matamshi yake yanaweza kuathiri mshikamano wa kitaifa.
Aidha, viongozi hao wameendeleza kampeni ya kuunga mkono ajenda ya Rais Ruto ya 'Usawa ni Sawa', wakisema serikali ya sasa imekuwa ikisambaza miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya nchi bila kuzingatia tofauti za kikabila au kijiografia.
Wamedai kuwa miradi ya barabara, nyumba za gharama nafuu, masoko ya kisasa na ajira ni baadhi ya maeneo wanayotaja kama ushahidi wa utendaji wa serikali ya Kenya Kwanza.
Wabunge hao wamesema sababu ya kuendelea kumuunga mkono Ruto ni rekodi yake ya maendeleo, wakidai kuwa uongozi wake umefungua fursa kwa jamii mbalimbali kushiriki katika maendeleo ya taifa.
Miongoni mwa waliozungumzia masuala hayo ni Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang'ula, msaidizi wa Rais Farouk Kibet, Mbunge wa Kitutu Chache North Japheth Nyakundi, Mbunge wa South Mugirango Sylvanus Osoro na Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago.
Wengine ni Joash Nyamoko, Jerusha Momanyi, Mbunge Mteule Irene Mayaka na Mbunge wa Taveta John Bwire.
Wetang'ula amekuwa akisisitiza kuwa IEBC ni taasisi huru kikatiba na inapaswa kupewa nafasi ya kutekeleza majukumu yake bila kuamuliwa na wanasiasa.
Kwa upande wake, Farouk Kibet amekuwa akimkosoa Gachagua kuhusu matamshi yake dhidi ya tume hiyo, akimtaka kuelekeza nguvu katika kuhamasisha wananchi kujisajili kama wapiga kura badala ya kuitisha maandamano dhidi ya IEBC.
Huku uchaguzi wa mwaka 2027 ukikaribia, mvutano kuhusu maandalizi ya uchaguzi, uhuru wa IEBC na mwelekeo wa kisiasa wa viongozi wa serikali na upinzani unaendelea kuwa sehemu muhimu ya mijadala ya kisiasa nchini Kenya.









