Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameiagiza Serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu makadirio ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, baada ya kubainika kutokuwepo kwa makubaliano kuhusu gharama za mradi huo.

Samia amesema kutokubaliana kati ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na mshauri elekezi kuhusu ukubwa wa bajeti kumekuwa kikwazo cha kuanza kwa kazi za ukarabati, licha ya muda wa maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kuendelea kuyoyoma.

Akizungumza Ijumaa, Novemba 27, 2026, katika hafla ya kuwaapisha mawaziri na viongozi wengine wa Serikali Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia alieleza kutoridhishwa na kuchelewa kwa mradi huo, akisema makadirio yaliyowasilishwa yanaonekana kuwa makubwa kiasi cha mshauri elekezi kushindwa kuyaidhinisha.

Kutokana na hali hiyo, amemuagiza Katibu Mkuu mpya wa Wizara hiyo, Abdallah Hassan Mitawi, kushirikiana na Waziri Paul Makonda kutafuta suluhu ya mvutano huo ili kazi ianze bila kuchelewa zaidi.

Aidha, Rais Samia amemwelekeza Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Moses Kusiluka, kuunda timu ya wataalamu wa uhandisi itakayopitia upya makadirio ya gharama za ukarabati huo na kubaini iwapo fedha zilizoombwa zinaendana na mahitaji halisi ya mradi.

Amesisitiza kuwa endapo uchunguzi utabaini gharama hizo zina msingi wa kitaalamu, mradi uendelee, lakini kama zimezidishwa, makadirio yafanyiwe marekebisho ili kuwezesha kazi kuanza.

Rais huyo amesema Tanzania haiwezi kuendelea kupoteza muda wakati Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likisubiri kuona uwanja huo ukiwa tayari kwa ukaguzi wa kukidhi viwango vinavyohitajika kabla ya mashindano hayo.

Uwanja wa Benjamin Mkapa ni miongoni mwa miundombinu muhimu inayotarajiwa kutumika katika AFCON 2027, ambayo Tanzania itaandaa kwa pamoja na Kenya na Uganda kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027.

Hata hivyo, changamoto za gharama na usimamizi wa miradi ya viwanja zimekuwa zikizua maswali kuhusu matumizi ya fedha za umma.

Awali, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilibaini dosari mbalimbali katika miradi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Benjamin Mkapa, Uhuru na Arusha, ikiwemo malipo ya kazi ambazo hazikutekelezwa, kasoro za vifaa na ongezeko la gharama za miradi.

Kamati hiyo iliitaka Serikali kuchunguza dosari hizo, kurejesha fedha zilizolipwa kinyume cha utaratibu na kuwawajibisha waliohusika.

Maagizo mapya ya Rais Samia yanakuja wakati Tanzania ikiendelea kuharakisha maandalizi ya AFCON 2027, mashindano yatakayokuwa ya kihistoria kwa Afrika Mashariki kutokana na ushirikiano wa nchi hizo tatu katika kuyaandaa.