Mahakama Kuu mjini Mombasa imempata mhubiri Paul Nthenge Mackenzie na washukiwa wengine 29 na hatia ya kuua bila kukusudia (manslaughter) kufuatia vifo vya wafuasi wao katika msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi.
Katika hukumu iliyotolewa Alhamisi, Novemba 27, 2026, Jaji Alex Ithuku alimkuta Mackenzie, ambaye alikuwa kiongozi wa kanisa la Good News International, pamoja na washukiwa wengine 18 na hatia ya makosa 123 ya kuua bila kukusudia kila mmoja.
Washukiwa wengine 10 walipatikana na hatia ya makosa 104 kila mmoja, yanayohusiana na kushiriki katika makubaliano ya pamoja ya kujiua kwa kujinyima chakula. Miongoni mwa waliopatikana na hatia ni mke wa Mackenzie, Rhoda Mumbua Maweu, aliyepatikana na hatia ya shtaka moja.
Katika uamuzi wake, mahakama ilibaini kuwa Mackenzie aliwashawishi wafuasi wake kwa utaratibu kujinyima chakula hadi kufa wakiamini kuwa wangekutana na Yesu.
Mahakama ilielezwa kuwa mpango huo ulitaka watoto waanze kufa kwanza, wakifuatiwa na wanawake na hatimaye wanaume, huku Mackenzie akipangiwa kuwa mtu wa mwisho kufariki.
Hata hivyo, mahakama iliwaachilia huru washukiwa 60 dhidi ya mashtaka yote, huku kesi dhidi ya wengine watatu ikisitishwa kutokana na vifo vyao wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) imesema inakusudia kukata rufaa kupinga kuachiliwa huru kwa baadhi ya washukiwa hao.
Hukumu hiyo inafuatia kesi iliyoanza Januari 23, 2024, ambapo upande wa mashtaka uliwaita mashahidi 95 na kuwasilisha vielelezo visivyopungua 375 kuthibitisha madai dhidi ya washtakiwa.
Uchunguzi wa maiti ulionyesha kuwa watu 129 kati ya waathiriwa 238 walifariki kutokana na njaa, huku miili ya wengine 86 ikiwa imesalia mifupa kiasi kwamba haikuwezekana kubaini chanzo cha vifo vyao.
Mashahidi waliambia mahakama kuwa Mackenzie alikuwa akihubiri dhidi ya elimu, matibabu na mapambo, akivielezea kuwa dhambi. Pia alidaiwa kuuita msitu huo Jangwani na kuyapa maeneo mbalimbali majina yanayotokana na Biblia.
Kwa upande wao, washtakiwa walijitetea kuwa walikwenda Shakahola kwa ajili ya kununua ardhi na kwamba kufunga kwao kulikuwa uamuzi wao binafsi.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ulisisitiza kuwa uhuru wa kuabudu hauwezi kutumiwa kuhalalisha vitendo vinavyosababisha vifo vya watu.
Mahakama sasa itasikiliza maoni ya waathiriwa, familia za marehemu, upande wa mashtaka na utetezi kabla ya kutoa hukumu ya adhabu.
Hukumu hiyo ni ya nne kwa Mackenzie ndani ya wiki moja, baada ya kupatikana na hatia katika kesi zinazohusiana na vifo vya watoto na ugaidi wa Shakahola.
Awali, Mahakama Kuu ya Mombasa ilikuwa imemhukumu kifungo cha miaka 200 jela kutokana na mauaji ya watoto 190 na mtu mzima mmoja.









