Maafisa wa usalama wamewaokoa raia 65 wa Ethiopia waliopatikana katika nyumba moja eneo la Mihang’o, Nairobi.

Watu hao baadhi wamenonekana kuwa katika hali dhaifu ya kiafya na kudhoofika kwa mwili.

Raia hao wanaripotiwa kuwa na dalili za utapiamlo, huku maafisa wa polisi wakiwakamata raia watatu wa Kenya kwa mahojiano kuhusiana na tuhuma za biashara haramu ya binadamu.

Uchunguzi umeanzishwa kubaini mazingira yaliyowafanya raia hao kupatikana katika nyumba hiyo, pamoja na kufichua iwapo kuna watu wengine waliohusika katika shughuli hiyo inayoshukiwa kuwa ya uhalifu.

Maafisa wa usalama wamewataka wananchi kuwa macho na kuripoti visa vinavyoweza kuashiria biashara haramu ya binadamu, ikiwemo watu kufungiwa ndani ya nyumba za makazi, msongamano usio wa kawaida katika majengo yenye vizuizi vya kutembea kwa uhuru, pamoja na watu wanaoonekana kudhoofika kiafya au kuwa katika hali ya dhiki.

Wamiliki wa nyumba, wasimamizi wa majengo, walezi na wakazi wametakiwa kufichua taarifa za kuaminika kuhusu tuhuma za kuwafungia watu kinyume cha sheria, kuwanyonya au kuwahusisha katika biashara haramu ya binadamu kwa mamlaka husika.

Hata hivyo, wananchi wameaswa kutoa ripoti kwa mamlaka husika kuhusiana na utaifa wake, mwonekano au uwepo wa wageni wasiowafahamu kwenye maeneo.

Aidha, wananchi wamehimizwa kutokabiliana na washukiwa wenyewe au kujaribu kuwaokoa watu wanaoshukiwa kuwa wahanga bila usaidizi wa mamlaka, kwani hatua hizo zinaweza kuhatarisha maisha ya wahanga na kutatiza uchunguzi.

Aidha wananchi wameombwa kuepuka kusambaza picha, majina au taarifa zisizothibitishwa kuhusu wahanga kwenye mitandao ya kijamii, ili kulinda usalama na utu wao.

Vilevile imesemekana kwamba kwa mtu yeyote aliye na taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi amehimizwa kuziwasilisha kwa polisi kwa siri na kuruhusu maafisa wa usalama kuchukua hatua zinazofaa.

Suala la raia wa kigeni kukutwa wakiwa wamedungiwa kwenye vyumba maalum si geni nchini huku mamlaka husika zikiweka mikakati kabambe ili utaratibu unaotakiwa ufuatwe na hata wahusika wafikishwe mbele ya vyombo vya kisheria kujibu mashtaka ya biashara haramu ya ulanguzi wa binadamu,kosa ambalo ni la jinai kote duniani.