Takribani watu 17 wamejeruhiwa kufuatia ajali ya barabarani iliyohusisha gari walimokuwa wakisafiria katika eneo la Migaa, kando ya barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.
Ajali hiyo ilitokea mapema Jumapili, Oktoba 18, 2026, majira ya saa sita na nusu usiku, huku waathiriwa wakipata majeraha ya viwango tofauti.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, gari hilo lilikuwa limewabeba waombolezaji waliokuwa wakisafiri kutoka jijini Kisumu kabla ya kuhusika katika ajali hiyo.
Hata hivyo, chanzo cha ajali hiyo hakijawekwa wazi kufikia sasa.
Tukio hilo lilizua hali ya taharuki miongoni mwa watumiaji wa barabara hiyo, huku juhudi za uokoaji zikianzishwa mara moja ili kuwasaidia waliojeruhiwa na kuhakikisha wanapata matibabu ya haraka.
Timu za uokoaji kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya, tawi la Nakuru, kwa ushirikiano na maafisa wa polisi pamoja na gari la dharura kutoka mjini Molo, zilifika eneo la tukio na kuendesha shughuli za uokoaji.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Shirika la Msalaba Mwekundu kupitia mitandao yake ya kijamii, mmoja wa majeruhi alikuwa amekwama ndani ya gari hilo kwa zaidi ya saa moja, hali iliyohitaji juhudi za ziada kutoka kwa waokoaji ili kumtoa salama.
Shirika hilo lilisema kuwa juhudi za kumwokoa majeruhi huyo zilifanikiwa, huku waathiriwa wote wakipata nafasi ya kusafirishwa hadi hospitalini kwa ajili ya kupokea matibabu.
“Majeruhi wote wamepata nafasi ya kukimbizwa hospitalini. Mtu mmoja alikuwa amekwama ndani ya gari hilo, ingawa tulipambana kumnusuru,” ilisema sehemu ya taarifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu.
Wakati wa shughuli za uokoaji, msongamano mkubwa wa magari uliripotiwa katika barabara hiyo, na kusababisha usumbufu kwa madereva na abiria waliokuwa wakielekea maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, maafisa wa usalama barabarani walifika eneo hilo na kuchukua hatua za kudhibiti hali, hatua iliyosaidia kurejesha mtiririko wa kawaida wa magari baada ya shughuli za uokoaji kuendelea.
Ajali hiyo inaongeza wasiwasi kuhusu usalama wa watumiaji wa barabara kuu zinazounganisha maeneo mbalimbali nchini, hasa nyakati za usiku ambapo mwonekano unaweza kuwa mdogo na madereva kukabiliwa na changamoto mbalimbali.
Hata hivyo, hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu hali ya kiafya ya majeruhi hao au iwapo kuna hatua zozote za kisheria zilizohukuliwa kufuatia tukio hilo.
Uchunguzi zaidi unatarajiwa kubaini mazingira kamili yaliyochangia kutokea kwa ajali h









