Watahiniwa watatu kutoka Kaunti ya Kwale watalazimika kufanya mitihani yao ya kitaifa wakiwa gerezani baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa kutumia nguvu.
Huku zikiwa zimesalia siku saba kabla ya kuanza kwa mitihani hiyo, wawili kati ya watahiniwa hao ni wa Gredi ya Tisa wanaotarajiwa kufanya mtihani wa KJSEA, huku mwingine akiwa wa Gredi ya Sita anayetarajiwa kufanya mtihani wa KPSEA.
Akizungumza na wanahabari afisini mwake, Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Kwale, Ahmed Abdi, alisema watahiniwa hao wanatoka maeneo bunge ya Matuga na Lungalunga.
Abdi alisema wawili kati yao wanatoka eneo bunge la Matuga, huku mwanafunzi mwingine akitoka Lungalunga.
Alisema hatua zimechukuliwa kuhakikisha kuwa watahiniwa hao wanapata nafasi ya kufanya mitihani yao licha ya kukabiliwa na changamoto za kisheria zilizowafanya kuwekwa gerezani.
Mkurugenzi huyo alifichua kuwa watahiniwa hao wamepokea huduma za ushauri nasaha ili kuwaandaa kisaikolojia na kuwasaidia kukabiliana na shinikizo la kufanya mitihani katika mazingira tofauti na yale ya wanafunzi wenzao.
Aidha, alisema idara ya elimu kwa ushirikiano na maafisa wa usalama imeweka mikakati ya kuhakikisha mitihani hiyo inaendeshwa kwa utaratibu unaofaa, huku usalama na usiri wa mitihani ukizingatiwa.
Alisema maandalizi hayo yanalenga kuhakikisha kuwa watahiniwa hao wanapata mazingira yanayowawezesha kujibu maswali yao bila vikwazo visivyo vya lazima.
Wakati huo huo, shule na vituo mbalimbali nchini vinaendelea na maandalizi ya mitihani ya KPSEA, KJSEA na KCSE, huku maafisa wa elimu wakisisitiza umuhimu wa kuzingatia kanuni za Baraza la Kitaifa la Mitihani nchini Kenya (KNEC).
Mitihani hiyo ni hatua muhimu katika safari ya kielimu ya wanafunzi, huku matokeo yake yakisaidia kutathmini maendeleo yao na kuwaelekeza katika hatua zinazofuata za masomo.
Kesi ya watahiniwa hao inaangazia changamoto zinazoweza kuwakabili wanafunzi wanapojikuta katika mazingira ya kisheria yanayoweza kuvuruga masomo yao.
Suala la watahiniwa kufanya mitihani yao nje ya mazingira ya shule,si jambo geni kwani baadhi wameshuhudiwa wakiwa kwenye vyumba vya kujifungua wakati wa zoezi lenyewe la mtihani,likiendelea katika vyumba vya shule.









