Taharuki imetanda katika eneo la Kasese, kaunti ndogo ya Muhoroni, baada ya mtu mmoja kufariki baada ya kugongwa na gari Alhamisi,Oktoba 15,2026.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, ajali hiyo ilihusisha lori lililokuwa linaendeshwa kwa kasi.

Tukio hilo limeibua hasira miongoni mwa wakazi, ambao baadaye walichoma moto malori manne kwa kule walichokidai kwamba madereva wamejenga mazoea ya kuendesha magari kiholela.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, marehemu alikuwa amesimama kando ya barabara wakati lori hilo lilipomgonga, na kusababisha kifo chake papo hapo.

Inadaiwa kuwa ajali hiyo ilitokea wakati magari yalipokuwa yakijaribu kupishana kwa kuyapita mengine kwa mwendo wa kasi, huku magari mawili yakikaribiana kutoka pande tofauti za barabara.

Hali hiyo inadaiwa kusababisha ajali hiyo ya kusikitisha, ambayo imezidisha wasiwasi kuhusu usalama wa watumiaji wa barabara katika eneo hilo.

Baada ya tukio hilo, wakazi waliokasirishwa na kifo hicho walichukua hatua ya kuchoma moto malori manne, wakidai kuwa magari hayo yamekuwa yakiendeshwa kwa kasi ya juu mara kwa mara bila kujali usalama wa watu wanaoishi na kufanya shughuli zao kando ya barabara.

Malori hayo hutumika kusafirisha vifaa vya ujenzi vinavyohitajika katika miradi ya ujenzi wa barabara inayoendelea katika eneo hilo.

Wakazi wanasema kuwa malori hayo yamekuwa yakionekana yakikimbia kwa kasi, hali inayodaiwa kuhatarisha maisha ya watembea kwa miguu pamoja na watumiaji wengine wa barabara.

Tukio hilo linaibua maswali kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhakikisha madereva wa magari ya mizigo wanazingatia sheria za barabarani, hasa katika maeneo yenye makazi ya watu na shughuli nyingi za kijamii.

Hata hivyo, maelezo zaidi kuhusu utambulisho wa marehemu, hatua zilizochukuliwa na polisi pamoja na iwapo kuna watu waliokamatwa kuhusiana na uchomaji wa malori hayo hayakuwa yamebainika katika taarifa za awali.

Vile vile, katika siku za hivi karibuni, imedaiwa kwamba baadhi ya magari ya kupakia mchanga na mawe yqmekuwa yakikiuka sheria na taratibu za matumizi ya barabara kote nchini

Wito umetolewa kwa madereva kuzingatia viwango vya mwendo vinavyoruhusiwa na kwa mamlaka husika kuimarisha usimamizi wa usalama barabarani ili kuzuia ajali zaidi.