Wananchi wa Migori, sasa wanaiomba serikali kuu na ile ya kaunti, kufanya hima katika kujenga daraja la mto Migori.
Wananchi wanasema wamekuwa wakipitia changamoto nyingi hususan wakati wa siku za soko, kwani inawalazimu kupiga foleni ili kuvuka kutoka pande moja hadi ya pili kutokana na idadi kubwa ya watu.
Aidha, wanadai serikali ilipaswa kuangazia ujenzi wa Daraja hilo kama kipau mbele kwani limesababisha adha kubwa miongoni mwa wananchi.
Brian Odhiambo, mwendesha pikipiki maarufu kama bodaboda, anasema kipato chake kimepungua mara kadhaa kutokana na kukosa namna ya kuwapakia wateja wake kutoka eneo la Namba hadi Posta kama ilivyokuwa.
Anasema inamlazimu apakie wateja kutoka Namba na kuwashushia eneo la Bansi ili wapange foleni ya kuvuka daraja kuelekea maeneo ya Posta, jambo abalo kulingana naye, limemkosesha kipato kwa maana ya nauli kushuka kama ilivyokuwa hapo awali.
Kwa upande wa abiria wanaotoka Isibania kuelekea Migori, wanasema changamoto zimeongezeka hususan kwa wale wanaoenda kutafuta matibabu katika hospitali kuu ya Migori au Huduma Centre.Hawa wanalazimika kupanda gari za kukodisha (tax) ili kuwapeleka moja kwa moja kutoka Migori ya Magharibi hadi Mashariki kwa kuzunguka Ojele, ambayo ndio njia mmbala iliyopendekezwa na serikali, kwa muda mfupi.
Hata hivyo wafanyabiashara ya uchukuzi wa umma wanasema imekuwa vigumu zaidi kupakia abiria wa Migori mjini kwani wapo wanaodai kushukia upande wa pili, kitendo kinachowalazimu kuzunguka kilometa kadhaa kabla ya kuwasili, huku nauli ikisalia kuwa ile ile.
Inakumbukwa kwamba daraja la Migori lilisombwa na mvua kubwa iliosababisha kuvunjika kwa kingo zake miezi kadhaa iliopita, hali iliosabaisha changamoto kubwa katika kuendesha shughuli mbalimbali zikiwemo za kiuchumi.
Hata hivyo gavana wa eneo hilo, Ochilo Ayacko amekaririwa akisema serikali haijasahau ujenzi wa daraja hilo muhimu kwani tayari mchakato unaendelea ili kunusuru wajasiriamali kuendelea na shughuli zao.
Daraja hilo la Mto Migori limeunga mji huo upande wa magahribi na mashariki, ambao pia ni makao makuu ya kaunti ya Migori inayozibeba zaidi ya wadi sita.
Ofisi za gavana, naibu wake, hospitali kuu ya kaunti na hata huduma centre, vyote vinapatikana upande wa mashariki, ukiwa unatokea magahribi na hivyo ni lazima mwananchi avuke mto kupitia kwa daraja au mbinu mmbadala ya kuzunguka Ojele.









