Wakaazi wa Kutus katika kaunti ya Kirinyaga, kwa ushirikiano na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kirinyaga, wamekesha katika maporomoko ya maji ya Kutus kando ya mto Thiba wakimtafuta mwanafunzi wa mwaka wa kwanza aliyeripotiwa kuzama Jumapili alasiri.

Maafisa wa polisi kutoka kituo cha Kutus, machifu na wasaidizi wao adiha wameshiriki kwenye juhudi za utafutaji hadi saa moja usiku, kufuatia taarifa za kusikitisha kuhusu mwanafunzi huyo kuzama majini.

Wazamiaji wa eneo hilo, wakiongozwa na Maulid Asman, wamesema juhudi za kumrejesha mwanafunzi huyo zinaendelea licha ya changamoto zinazotokana na kina kirefu cha maji na mkondo mkali wa mto huo.

Asman anasema baadhi ya maeneo ya maporomoko hayo yana kina kirefu, huku mizizi ya miti iliyo ndani ya maji ikiongeza hatari kwa wanaojaribu kupiga mbizi kumtafuta mwanafunzi huyo.

“Mkondo wa maji una nguvu sana, na kuna maeneo ambayo mtu anaweza kuzama. Pia kuna mizizi mingi ya miti inayoweza kumnasa mtu. Hata sisi tunaohusika na utafutaji tuna hofu ya kupoteza maisha,” Asman.

Wanafunzi wenzake wamesema marehemu alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza ambaye alijiunga na chuo hicho mwezi Septemba mwaka huu.

Mmoja wa wanafunzi hao anasema ni jambo la kusikitisha kwamba mwanafunzi huyo amekumbwa na mkasa huo muda mfupi baada ya kuanza maisha yake ya chuo kikuu.

Maafisa wa usalama waliokuwa katika eneo la tukio walisema mwanafunzi huyo anatoka Lodwar na kwamba familia yake ilikuwa tayari imearifiwa kuhusu mkasa huo.

Kwa mujibu wa mmoja wa maafisa hao, mwanafunzi huyo alikuwa akiogelea na rafiki yake alipojaribu kumsaidia, lakini naye akashindwa kujinasua majini.

Wakaazi wa Kutus wamesema si mara ya kwanza kwa watu kuzama katika maporomoko hayo, wakitaka mamlaka husika kuweka mabango ya tahadhari ili kuwaonya wanafunzi na wageni kuhusu hatari zilizopo.

Joseph Wachira, mkazi wa Kutus, anasema eneo hilo ni mojawapo ya vivutio vya kimaumbile katika kaunti ya Kirinyaga vinavyowavutia wageni kutoka maeneo mbalimbali.

Wanafunzi na wakaazi hao wameahidi kuendelea na utafutaji huku wakisubiri familia ya mwanafunzi huyo kufika na juhudi za kurejesha mwili wake zikikamilishwa.