Wakenya 52 Watajwa Orodha ya Wahamiaji Wanaolengwa Marekani

Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump umesema umefuta zaidi ya visa 300,000 tangu kuanza kwa operesheni yake ya kuimarisha utekelezaji wa sheria za uhamiaji nchini humo.

Wakenya ni miongoni mwa watu walioathiriwa na hatua hiyo, huku utawala wa Trump ukiwa umeorodhesha Wakenya 52 katika hifadhidata ya Idara ya Usalama wa Nchi ya Marekani (DHS) inayowataja wahamiaji wanaolengwa kuondolewa nchini humo kama “wahalifu hatari zaidi.”

Taarifa hiyo inaonyesha kuwa visa vya maelfu ya watu vimebatilishwa katika kipindi ambacho serikali ya Marekani imeongeza ukaguzi dhidi ya wahamiaji na wageni wanaodaiwa kukiuka masharti ya visa zao.

Hatua hiyo imezua wasiwasi miongoni mwa Wakenya wanaoishi Marekani, pamoja na wale wanaopanga kusafiri kwenda nchini humo, huku baadhi yao wakihofia kuathiriwa na ukaguzi mkali katika vituo vya kuingilia nchini Marekani.

Idara ya Usalama wa Nchi imekuwa ikitumia hifadhidata hiyo kufuatilia watu wanaodaiwa kuwa na historia ya uhalifu au wanaotajwa kuwa wanastahili kuondolewa nchini humo.

Kulingana na taarifa za utawala huo, watu waliolengwa ni pamoja na wale wanaodaiwa kukiuka sheria za uhamiaji, kufanya uhalifu au kukiuka masharti yaliyowekwa kwenye visa zao.

Hata hivyo, haijabainika mara moja ni visa vingapi vya Wakenya vilivyofutwa wala ni watu wangapi kati ya waliotajwa katika hifadhidata hiyo ambao tayari wameondolewa nchini Marekani.

Hatua hiyo inajiri wakati utawala wa Trump ukiendelea kutekeleza sera kali za uhamiaji, ikiwemo kuimarisha ukamataji na uhamishaji wa wahamiaji wasio na vibali halali.

Wakenya wanaoishi Marekani wamehimizwa kufuatilia hali ya visa zao na kuhakikisha kuwa wanafuata masharti yote ya uhamiaji ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria au kuondolewa nchini humo.

Hii ni mara ya nne ndani ya kipindi cha miaka miwili kutokea kwa tamko hilo kutoka nchi ya Marekani kuwafutia wananchi hati za usafiri kwa madai kwamba kuna baadhi ya mataifa yana sifa za kigaidi.
Hali hii inaathiri watu wengi hususan wale wanaohitaji huduma ikiwemo masomo na hata matibabu mbalimbali.