Sintofahamu imeibuka katika kanisa la AIC Kayole North jijini Nairobi, baada ya baadhi ya waumini kupinga uongozi wa mchungaji.
Mchungaji huyo aliyefahamika kama Makau, waumini sasa wanamtaka ahamishwe kutokana na madai ya uongozi wa kimabavu na majivuno.
Waumini hao wanaeleza kwamba wamekuwa wakilalamikia uongozi wa mchungaji huyo kwa muda, wakidai kuwa hawapewi nafasi ya kutosha kushiriki katika maamuzi na shughuli za maendeleo ya kanisa.
Wanasema wamewasilisha malalamishi yao kwa kamati kuu ya kanisa, lakini madai yao hayajashughulikiwa ipasavyo.
Kwa mujibu wa waumini hao, waliambiwa kuwa uhamisho wa mchungaji huyo umekuwa mgumu kutokana na kiwango chake cha mshahara, ambacho wanadai ni cha juu ikilinganishwa na cha wachungaji wa matawi mengine jijini Nairobi.
Aidha Jumapili ya Oktoba 18,2026, asubuhi, baadhi ya waumini walibaki nje ya kanisa kwa muda mrefu milango ikiwa imefungwa.
Waumini hao aidha wamebeba mabango yenye ujumbe uliosomeka, “Rev Makau Must Go,” wakitaka mchungaji huyo aondolewe katika tawi hilo.
Viongozi vijana wa kanisa hilo wanadai kuwa mawazo yao kuhusu maendeleo ya kanisa yamekuwa yakipuuzwa, huku wakidai kunyimwa ufikiaji wa fedha za kanisa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali.
Wanafafanua kwamba hali hiyo imewafanya kuhisi kutengwa katika shughuli za uongozi, wakitaka kuwepo kwa uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa waumini katika maamuzi yanayohusu kanisa.
Aidha, waumini hao wanaitaka uongozi wa AIC kuweka utaratibu ulio wazi wa usimamizi na matumizi ya rasilimali za kanisa, wakipinga kile wanachodai kuwa maamuzi muhimu kufanywa na watu wachache bila kuwashirikisha wengine.
Waumini hao pia wametaka uongozi wa kanisa kutoa ufafanuzi kuhusu matokeo ya ripoti ya baraza la usuluhishi (tribunal), ambayo wanadai ilipendekeza uhamisho wa baadhi ya viongozi wa kanisa.
Wamehoji hatua zilizochukuliwa kutekeleza mapendekezo hayo, wakitaka mamlaka husika za kanisa kuingilia kati na kutafuta suluhu ya kudumu kupitia mazungumzo.
Waandamanaji hao wamesema kusuluhishwa kwa mzozo huo kutasaidia kurejesha imani miongoni mwa waumini na kuimarisha umoja wa kanisa, huku wakisisitiza kuwa wanataka mazingira yatakayowaruhusu kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiroho za kanisa.
Majibu ya uongozi wa kanisa kuhusu malalamishi hayo hayakuwa yamepatikana kufikia wakati wa usilishwaji wa taarida hii.









