Serikali ya Kenya,inalenga kuongeza kiwango cha bidhaa zinazotengenezwa nchini na kutumiwa na Wakenya kutoka asilimia 30 hadi 50. Hatua hiyo inalenga kukuza viwanda na kutengeneza nafasi zaidi za kazi.
Katibu Mkuu katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Juma Mukhwana, amesema Kenya inapaswa kuacha kutegemea zaidi kuuza nje malighafi na badala yake kuongeza uzalishaji na uchakataji wa bidhaa nchini.
Mukhwana anasema karibu asilimia 70 ya bidhaa zinazotumiwa nchini huagizwa kutoka nje. Amehimiza kuongezwa kwa uzalishaji wa ndani ili kupunguza utegemezi wa uagizaji na kuhifadhi nafasi za kazi nchini.
Kenya pia inalenga kukuza mchango wake katika bidhaa zinazosambazwa chini ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), ambao kwa sasa ni asilimia 16, ili kufungua masoko zaidi kwa wazalishaji wa ndani.
Katika hatua nyingine jumuiya ya Afrika mashariki (EAC) inaongeza juhudi za kukuza biashara ya mtandaoni na biashara ya kidijitali baina ya nchi wanachama. Juhudi hizo zinajumuisha kuboresha kanuni, kulinda wateja na kuimarisha mifumo ya malipo ya kidijitali.
Hatua hiyo inatarajiwa kupanua masoko kwa biashara, hasa biashara ndogo na za kati, na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi katika eneo hili.
Biashara baina ya nchi wanachama wa EAC imeongezeka kutoka takriban shilingi bilioni 207 mwaka 2005 hadi shilingi trilioni 2.54 mwaka 2025, ishara ya kuongezeka kwa fursa za biashara ya kidijitali.
Jumuiya hiyo pia inafanya kazi ya kuoanisha mifumo ya ulinzi wa watumiaji, kuboresha usalama wa mtandao na kuimarisha miundombinu ya kidijitali.
Lengo ni kuweka mazingira salama na ya kuaminika kwa miamala ya mtandaoni.
Benki ya Dunia yaonya kuhusu pengo la ajira milioni 800 duniani.
Wakati huo huo, rais wa Benki ya Dunia, Ajay Banga, ameonya kuwa dunia inaweza kukabiliwa na upungufu wa ajira milioni 800, huku vijana bilioni 1.2 wakitarajiwa kuingia katika soko la ajira katika kipindi cha miaka 10 hadi 15 ijayo.
Akizungumza katika Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na shirika la fedha la kimataifa (IMF) mjini Bangkok, Banga ametoa wito wa kuongeza uwekezaji katika miundombinu, nishati, kilimo na biashara ndogo ili kuharakisha uundaji wa nafasi za kazi.
Amesema Benki ya Dunia ilichochea upatikanaji wa mtaji wa kibinafsi wa dola bilioni 112 mwaka jana, kutoka dola bilioni 35 mwaka 2022, kusaidia maendeleo na ukuaji wa uchumi.









