R9ais William Ruto anatarajiwa kukabidhi uenyekiti wa Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) kwa Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa.

Ni wakati viongozi wa mataifa 21 wanapokutana mjini Harare kujadili mikakati ya kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo ya viwanda katika eneo hilo.

Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa COMESA unafanyika Alhamisi, Oktoba 22, 2026, ukiwaleta pamoja viongozi kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kuondoa vikwazo vya kibiashara na kufungua fursa mpya za uwekezaji katika mataifa wanachama.

Zimbabwe inatarajiwa kuchukua uenyekiti wa jumuiya hiyo kwa kipindi cha 2026–2027, huku Eswatini ikihudumu kama makamu mwenyekiti na Kenya ikichukua nafasi ya mratibu wa kumbukumbu za mkutano huo.

Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, ni miongoni mwa viongozi wengine wanaotarajiwa kushiriki mkutano huo unaoandaliwa na Mnangagwa.

Mkutano huo unaongozwa na kaulimbiu, “Soko Moja, Mustakabali Mmoja: Kuendeleza Ukuaji Jumuishi wa Viwanda, Uwekezaji na Muungano wa Kikanda ndani ya COMESA.”

Akizungumza baada ya kuwasili Harare, Ruto alisema viongozi watajadili kuimarisha muungano wa kikanda, kudumisha amani na usalama, kuharakisha utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) na kuongeza thamani ya rasilimali za Afrika ili kukuza uchumi.

Kwa Kenya, kuimarika kwa biashara ya kikanda kunaweza kufungua masoko mapya kwa bidhaa zinazozalishwa nchini, zikiwemo mazao ya kilimo, vyakula vilivyosindikwa na bidhaa za viwandani.

Kuondoa vikwazo vya kibiashara na kuboresha barabara, usafiri na miundombinu ya mipakani pia kunaweza kupunguza gharama za usafirishaji na kurahisisha biashara baina ya mataifa wanachama.

Viongozi hao wanatarajiwa pia kujadili namna ya kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo na madini badala ya kuendelea kuuza malighafi bila kuzichakata. Hatua hiyo inalenga kukuza viwanda vya ndani, kuongeza mapato na kuunda nafasi za ajira kwa wananchi.

Ajenda nyingine muhimu ni Mpango Mkakati wa COMESA wa Muda wa Kati wa 2026–2030, utakaotoa mwelekeo wa vipaumbele vya jumuiya hiyo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mpango huo unalenga kupanua biashara baina ya mataifa wanachama, kuimarisha miundombinu, kuendeleza teknolojia za kidijitali na kuboresha maisha ya wananchi.

Kabla ya mkutano wa wakuu wa nchi, Jukwaa la Biashara la COMESA liliwakutanisha wawekezaji, viongozi wa biashara na watunga sera kujadili upatikanaji wa mitaji, ushindani wa viwanda na uimarishaji wa minyororo ya thamani katika eneo hilo.

Kwa Zimbabwe, kuandaa mkutano huo kunatoa fursa ya kutangaza uwezo wake katika biashara, utalii na uwekezaji, huku ikijiandaa kuongoza jumuiya hiyo.

Kwa upande wa Kenya, kukabidhi uenyekiti kutahitimisha kipindi cha Ruto katika uongozi wa COMESA, ingawa nchi hiyo itaendelea kushiriki katika maamuzi ya jumuiya hiyo.

Hata hivyo, manufaa ya mkutano huo yatategemea utekelezaji wa maazimio yatakayofikiwa, kuondolewa kwa vikwazo vya biashara na uwezo wa serikali wanachama kubadilisha makubaliano ya kikanda kuwa fursa halisi kwa wafanyabiashara na wananchi.