Raila Alikuwa Rafiki na Hata Mwanademokrasia Halisi-Macharia
Siaya:Raila Amolo Odinga alikuwa Mkenya aliyejitolea katika kupigania maslahi ya taifa la Kenya, hayo ni kwa mujibu wa mwenyekiti wa Royal Media Services,(RMS) Dk SK Macharia.
Akizungumza katika ibada ya kumuenzi Raila iliyofanyika Oktoba 15, 2026, katika uwanja wa Migwena, Kaunti ya Siaya, Macharia alimwelezea kama mwanademokrasia aliyejitolea na Mkenya halisi.
Taarifa za kifo cha Raila, kilimgusa sehemu kubwa si kwake binafsi bali na familia na Kenya kwa ujumla wake.
“Familia hii inavyohisi kuhusu msiba huu, mimi na familia yangu pia tumempoteza rafiki mkubwa, Mkenya mkuu na rais ambaye Kenya ilimhitaji lakini haikuwahi kumpata,” alisema Macharia.
Alikumbuka kuwa alikuwa amesimama na Raila katika safari yake ya kisiasa, hata wakati wa nyakati ngumu. Macharia alisema urafiki wao ulithibitishwa na namna Raila alivyomjali baada ya kushindwa katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2022.
Kwa mujibu wa Macharia, Raila pamoja na kakake Oburu Oginga walimtembelea nyumbani kwake ili kumfariji. Alisema ziara hiyo ilimwonyesha kuwa Raila hakuwa mtu wa kusubiri wengine wamtafute tu wakati wa shida; yeye mwenyewe alichukua hatua kuwafariji waliokuwa wameumia.
“Katika uchaguzi wa 2022, Raila aliposhindwa, yeye na kakake Oburu walikuja nyumbani kwangu kunituliza. Si mimi niliyeenda kwa Raila. Ni yeye na kakake waliokuja nyumbani kwangu,” Dk Macharia.
Macharia alieleza kuwa uhusiano wake na familia ya Odinga ulianza kabla ya Raila kuingia katika nafasi za juu za uongozi. Alisimulia mkutano wake wa kwanza na babake Raila, Jaramogi Oginga Odinga, katika Hospitali Kuu ya Kisumu, wakati alipokuwa ameandamana na rais wa zamani Jomo Kenyatta.
Alisema alitambua mapema kuwa Jaramogi alikuwa mtu aliyejitolea kwa taifa. Baadaye, Jaramogi alimwomba aangalie wanawe Raila na Oburu iwapo yeye angefariki.
“Jaramogi aliniambia ana wana wawili, Oburu na Raila Odinga, na mimi ni mkubwa kuliko wao. Iwapo hataishi muda mrefu, niwatunze,” Macharia alikumbuka.
Alisema ombi hilo liliweka msingi wa uhusiano wa muda mrefu kati yake na ndugu hao pamoja na familia zao.
Macharia pia alisimulia jinsi alivyoendelea kumuunga mkono Raila katika kampeni zake huku akitolea mfano uchaguzi uliopita kwamba alimpa helikopta, rubani na mafuta ya kampeni kwa gharama yake mwenyewe.
“Unaweza kufikiria mtu wa hadhi yangu katika uchaguzi uliopita akimpa Raila helikopta, rubani na mafuta yote ya kufanya kampeni kwa gharama yangu,” alisema.
Kabla ya kifo chake, Raila alikuwa amemwomba Macharia aende Siaya kumsaidia Oburu katika shughuli iliyohusisha serikali ya kaunti. Macharia alisema Raila alimweleza kuwa alikuwa amemaliza safari yake na alikuwa anajisikia vizuri. Alitarajia kurejea Nairobi ndani ya siku mbili au tatu.
Mahusiano hayo yalifanya kifo chake kuwa cha kushtua zaidi kwa Macharia, ambaye alisema alikuwa amezungumza naye siku mbili tu, awali. Katika hotuba yake, alisisitiza kuwa Raila alikuwa kiongozi aliyejali demokrasia na maslahi ya Kenya—na kwa familia ya Macharia, alikuwa rafiki wa kweli ambaye pengo lake litahisiwa kwa muda mrefu.









