Polisi wameimarisha ulinzi katika Soko la Masinde Muliro mjini Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia, huku Gavana George Natembeya akipanga kulizuru eneo hilo Jumatatu, Oktoba 19, 2026, kufuatia mzozo unaozidi kuchacha kati yake na Rais William Ruto.

Vikosi vya usalama vimepelekwa katika soko hilo huku magari ya kunyunyizia maji yakionekana eneo hilo kabla ya ziara iliyopangwa na gavana huyo, ambaye amesisitiza kuwa atahakikisha wafanyabiashara wanaostahili wanapata nafasi za kufanya biashara katika soko hilo.

Mvutano huo unatokana na kutokubaliana kuhusu usimamizi wa soko hilo jipya, ambalo lilizinduliwa na Rais Ruto wakati wa ziara yake ya Trans Nzoia wiki iliyopita.

Natembeya amekuwa akipinga hatua ya serikali ya kitaifa kuhusika katika usimamizi wa miradi anayodai ilitekelezwa kwa kutumia rasilimali za serikali ya kaunti.

Gavana huyo anadai kuwa wafanyabiashara waliokuwa wamepangiwa nafasi katika soko hilo na serikali yake wanapaswa kupewa kipaumbele, akishutumu serikali ya kitaifa kwa kuingilia majukumu ya utawala wa kaunti.

Jumamosi, Natembeya alitangaza kuwa hatazuiliwa kutembelea soko hilo, akiwataka polisi kumkamata iwapo wanaamini ziara yake ni kinyume cha sheria.

Mzozo huo umeenea pia katika sekta ya afya baada ya Rais Ruto kutangaza mpango wa kujenga Hospitali ya Kitale Level 5 kwa gharama ya shilingi bilioni moja.

Natembeya amepinga mpango huo, akisema serikali ya kitaifa inapaswa kuheshimu ugatuzi na kushirikisha utawala wa kaunti katika miradi inayohusu ardhi na majukumu yake.

Hata hivyo, Rais Ruto amesema ataendelea na mpango wa kujenga hospitali hiyo licha ya tofauti zake za kisiasa na gavana huyo, akisisitiza kuwa mradi huo unanuiwa kuwahudumia wananchi.

Mvutano huo unajiri siku chache baada ya makabiliano kati ya makundi ya wafuasi wa kisiasa mjini Kitale, ambapo polisi waliripoti maafisa wawili kujeruhiwa na magari mawili ya serikali kuharibiwa.

Hali ya usalama katika soko hilo inatarajiwa kuangaziwa zaidi huku kukiwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa makabiliano wakati wa ziara ya gavana huyo.
Hata hivyo mzozo huo baadhi wanasema ni mtindo wa kisiasa nchini kenya ambapo mara baada ya kura, kila kitu kitarejea kwenye hali yake ya kawaida