Padri Patricio Alfredo Sánchez Molinari amefariki dunia baada ya kuangukiwa na msalaba mkubwa wa mbao wenye sanamu ya Yesu Kristo alipokuwa akiongoza ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa la Nuestra Señora del Perpetuo Socorro, Jijini Guayaquil, nchini Ecuador.
Tukio hilo limeripotiwa kutokea usiku wa Jumamosi, Oktoba 17, 2026, na kusababisha taharuki miongoni mwa waumini waliokuwa wakishiriki ibada hiyo.
Kwa mujibu wa maelezo ya tukio hilo, Padri huyo alikuwa akiongoza misa iliyokuwa ikitangazwa mubashara kupitia mitandao ya kijamii wakati msalaba uliokuwa ukining'inia ukutani nyuma ya madhabahu ulipoanguka ghafla na kumwangukia.
Tukio hilo lilinaswa katika matangazo hayo, huku sauti za waumini wakipiga mayowe zikisikika. Baadhi yao walikimbilia eneo la madhabahu kujaribu kumsaidia Padri huyo, huku wengine wakitafuta msaada wa haraka.
Jimbo Kuu Katoliki la Guayaquil lilithibitisha kifo cha Sánchez Molinari kupitia taarifa rasmi, likieleza masikitiko yake kutokana na msiba huo. Jimbo hilo lilitoa pole kwa familia ya kidini ya Redemptorists, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu, huku likiwaomba waumini kuungana katika maombi ya kuiombea roho yake ipumzike kwa amani.
Padri Sánchez Molinari alikuwa paroko wa kanisa hilo na mwanachama wa Shirika la Redemptorists, ambalo hujishughulisha na huduma za kiroho na uinjilidmsti.
Alikuwa akiongoza ibada za kila siku zilizokuwa zikitangazwa kupitia mitandao ya kijamii ili kuwafikia waumini wasioweza kuhudhuria kanisani.
Hadi taarifa za awali zilipotolewa, chanzo cha msalaba huo kujitoa ukutani hakikuwa kimefafanuliwa rasmi. Pia, hakukuwa na maelezo ya kutosha kuhusu hali ya mfumo uliokuwa umeushikilia au iwapo kulikuwa na hitilafu ya kiufundi iliyosababisha ajali hiyo.
Kifo cha Padri huyo kimeibua huzuni miongoni mwa waumini wa Kanisa Katoliki nchini Ecuador, huku video ya tukio hilo ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Tukio hilo limeacha maswali kuhusu mazingira yaliyosababisha msalaba huo mkubwa kuanguka wakati ibada ikiendelea.
Kifo cha padre huyo kimeibua maswali mengi likiwemo la uhakiki wa udhabiti wa msalaba huo,hapo kanisani na jinsi dalili hazikuweza kuonekana kabla ya mkasa mzima kutokea na kuzua umauti.









