Olayemi Afariki Dunia, Familia Yathibitisha
Lagos:Familia ya mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Nigeria, Olayemi Bayonile Bolaji, maarufu kama Toluwanisings, imethibitisha kifo chake na kuwaomba mashabiki na watu wengine kuwaombea mkewe, watoto wake na jamaa zake katika kipindi hiki cha maombolezo.
Katika taarifa, familia ilisema mwimbaji huyo aliaga dunia mapema Jumatano, Oktoba 14, 2026 na kwamba kifo chake ni pigo kubwa na chungu kwa watu wake wa karibu na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo familia haikutoa maelezo kuntu kuhusu chanzo cha kifo chake, na badala yake, ilisema itatangaza mipango ya mazishi baadaye na kuwaomba mashabiki na watu wenye mapenzi mema kuwaombea walioachwa na marehemu.
Taarifa hiyo ilisema Toluwanisings alikuwa “ameaga dunia,” huku familia ikiomba faragha na heshima inapoomboleza msiba huo.
Habari za kifo chake zilipoanza kusambaa, mashabiki wengi walieleza kutokuamini na kwamba zinlikuwa za kubabaisha tu mitandaoni.Mara baada ya familia kutoa taarifa kamili, salamu za rambi rambi zimemiminika kutoka kwa wadau mbali mbali wakiwemo wasanii wa muziki wa injili nchini humo na nje ya nchi ya Nigeria.
Miongoni mwa waliotoa salamu za rambirambi ni wakili Pelumi Olajengbesi na mchekeshaji Woli Agba. Awali, Woli Agba alikuwa ameomba watu wamwombee mwimbaji huyo, hatua iliyoongeza wasiwasi kuhusu hali yake kabla ya kutangazwa kwa kifo chake.
Toluwanisings alikuwa amejishughulisha na muziki kwa takriban miaka 11, akijenga wafuasi kupitia nyimbo za injili zilizopata umaarufu miongoni mwa mashabiki wake. Nyimbo zake zilizojulikana ni pamoja na Unreserved Praise, A Very Big God, Onibuore, E Lagbara na Owo Re Meji Meji.
Kupitia nyimbo na maonyesho yake, alipata kutambulika ndani ya muziki wa injili nchini Nigeria na miongoni mwa wasikilizaji wengine nje ya nchi hiyo. Mashabiki wanaendelea kukumbuka kazi zake na mchango wake katika muziki wa injili katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.
Kifo chake pia kimeibua kumbukumbu za ajali ya barabarani aliyohusika nayo miezi kadhaa iliyopita akiwa pamoja na baadhi ya wanamuziki wa bendi yake. Hata hivyo, taarifa zilizotolewa hazijaonyesha iwapo ajali hiyo ilihusiana na kifo chake.
Familia inatarajiwa kutoa taarifa zaidi kuhusu mazishi yake baadaye. Kwa sasa, imewaomba watu waendelee kuwaombea mkewe, watoto wake na jamaa wengine wanapopitia kipindi hiki cha majonzi.









