Kiongozi wa chama cha siasa nchini Kenya, People’s Party of Kenya (PPK), Ndindi Nyoro, ameishutumu serikali kwa kushindwa kusimama na wananchi dhidi ya kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta.

Aidha ameitaka mikataba ya sekta ya mafuta iwe wazi na kuomba upinzani kuungana katika kuelekea uchaguzi mkuu, nchini.

Kinara huyo wa PPK, ameshtumu ongezeko hilo la bei ya mfuta na kuinyooshea kidole serikali kwa kuruhusu watu wachache kunufaika, huku mamilioni ya wakenya wakitaabika.

Akizungumza katika makao makuu ya People’s Party of Kenya (PPK) na wadau mbalimbali wakiwemo wagombea watarajiwa wa nyadhifa mbalimbali na wananchama kutoka maeneno tofautitofauti ya nchi, akihoji na kusema ongezeko hilo lililotangazwa na mamlaka ya udhibiti wa nishati na petroli (EPRA) haliaksi uhalisia wa soko la kimataifa la nishati hiyo.

Aliipa serikali hadi mwishoni mwa wiki hii, kupunguza bei na kuishutumu EPRA kwa kuwapotosha wananchi kuhusu kupanda kwa gharama ya bidhaa za mafuta zinazoagizwa kutoka nje.

Nyoro pia alihoji mpango wa (G to G) wa kuagiza mafuta na kusema unalenga kunanufaisha kundi dogo la watu badala ya nchi, na kumtaka rais Ruto aeleze namna unavyowanufaisha wakenya huku akiongeza kwamba G to G ni mchongo wa kimkakati wa kuwanufaisha baadhi ya watu nchini na hivyo, unapaswa kufutiliwa mbali.

Katika hatua nyingine, alielezea wasiwasi wake kuhusiana na usimamizi wa rasilimali za mafuta, huko Turkana, akiongeza kwamba watu wa gatuzi la Turkana wanapaswa kuwa katika mstari wa mbele kwenye kunufaika.

Kuhusu mradi wa Dangote Oil Refineries huko Lamu, Nyoro alisema tayari kuna baadhi ya watu wachache wamepangwa kunufaika na huenda wana hisa kwenye mradi mzima wa Dangote, raia wa Nigeria.

Kuhusu maswala ya bunge, kinara huyo wa PPK alisema rais Ruto amejikita zaidi katika kuwashawishi wabunge, hali anayosema imeendelea kudhoofisha uwezo wa bunge kufanya kazi yake kwa uwazi na uhuru.

Nyoro alisema kusimamishwa kwake kushiriki vikao vya bunge la taifa, hakutamnyamazisha wala kubadili msimamo wake na ataendelea kutaka uwajibikaji.

Kwa upande wa siasa, Nyoro amewataka viongozi waache malumbano ya hadharani na badala yake wajikite katika kujenga muungano imara wa kuikabili serikali ya Kenya Kwanza kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Ni hapa ambapo Nyoro alihakikishia umma kwamba yeye sio mradi wa serikali kama anavyodai, Mbunge wa Naivasha, Jane Kihara na kusema hizo ni propaganda za kawaida kwake.