Raia wa Marekani wameonywa dhidi ya kutembelea baadhi ya maeneo nchini Kenya kutokana na hatari za uhalifu, utekaji nyara na ugaidi zinazoweza kuhatarisha usalama wao.

Onyo hilo linahusu maeneo kadhaa ya Nairobi,pwani na kaunti zilizo karibu na mipaka ya Kenya na nchi jirani, huku wasafiri wakishauriwa kuchukua tahadhari wanapopanga safari zao.

Katika mji mkuu wa Nairobi, raia hao wameonywa dhidi ya kutembelea vitongoji vya Eastleigh na Kibera kutokana na hatari ya uhalifu na utekaji nyara.

Eastleigh ni eneo lenye shughuli nyingi za kibiashara, huku Kibera ikiwa mojawapo ya makazi yenye msongamano mkubwa wa watu jijini Nairobi.

Aidha, onyo hilo linahusu kaunti za Garissa, Wajir na Mandera, pamoja na Lamu, Tana River na maeneo ya Kaunti ya Kilifi yaliyo kaskazini mwa Barabara Kuu ya C103.

Maeneo ya pwani yaliyo kaskazini mwa Malindi pia yametajwa kuwa na hatari zinazohusishwa na utekaji nyara na ugaidi.

Katika eneo la Bonde la Ufa, raia wa Marekani wameonywa dhidi ya kusafiri katika Kaunti ya West Pokot na sehemu za magharibi mwa Kaunti ya Turkana kutokana na hatari ya uhalifu.

Vilevile, tahadhari imetolewa kuhusu maeneo ya kaunti za Marsabit na Turkana yaliyo ndani ya umbali wa kilomita 50 kutoka mpaka wa Ethiopia, kutokana na hatari ya machafuko na ukosefu wa utulivu wa kiusalama.

Onyo la marekani dhidi ya raia wake si la kwanza barani Afrika,bali nchi hiyo imekuwa ikiwafuatilia raia wake hususan pale panapotokea taharuki ya kuzuka kwa utovu wa usalama.

Wakati wa uchaguzi mkuu uliopita nchini Tanzania,Marekaniilitoa onyo hadi katika ubalozi wake jijini Dar es Salaam kwamba nchi hiyo imekosa kujiendesha kidemokrasia na hivyo kuzua taharuki kubwa.

Tamko sawa la hilo limewahi kutolewa kwenye mataifa ya Sudan na Sudan Kusini wakati mataifa hayo yakiwa kwenye mgogoro mzito wa kutaka kugawana mikoa.

Hali hiyo ilisababisha Sudsn kugawanyika vipande viwili na kuzaa Sudan Kusini Na Sudan.
Marekani inasema baadhi ya viongozi barani Afrika,wameshindwa kudhibiti ugaidi na hivyo kuhatarisha maisha ya raia wao.