Makali Ya Mafuta Kenya Yang’ata Mbele na Nyuma

Watumiaji wa vyombo vya nishati ya mafuta aina ya Petroli nchini Kenya, watalazimika kuendana na hali ilivyo ya nyongeza ya bidhaa hiyo.Hii ni baada ya Mamlaka ya Nishati ya Petroli (EPRA) kutangaza viwango vipya vya bei.

Kwa mujibu wa mamlaka hayo, bei hizo zitatumika hadi Novemba 14, ambapo mjini Mombasa itakuwa na unafuu wakati jiji la Nairobi,Kisumu na Nakuru vikiongoza bendera ya makali ya kuimudu bei ya juu kutokana na mfumo wa kupata bidhaa hiyo adimu.
Aidha, nishati ya petroli sasa inauzwa kwa takriban Sh12 hadi Sh13 zaidi kwa lita ikilinganishwa na mwezi uliopita.Hata hivyo, kwenye matumizi ya mafuta taa, ongezeko hilo limepanda na kukaribia Shilingi 28, ndani ya miji ya Nakuru, Eldoret na Nairobi mtawalia.

Mombasa, ambayo ndiyo bandari kuu ya kuingiza mafuta nchini, ina viwango vya juu vya Sh223.81 kwa lita ya petroli, Sh224.61 kwa dizeli na Sh216.71 kwa mafuta ya taa. Bei hizo ni za chini zaidi ikilinganishwa na Nairobi, Nakuru, Kisumu na Eldoret.
Nairobi ina petroli ghali zaidi kati ya miji hiyo mitano, ikiwa Sh226.96 kwa lita. Dizeli inagharimu hadi Sh227.76, huku mafuta ya taa yakiwa Sh219.87. Hata hivyo, Kisumu na Eldoret zinaongoza kwa bei ya juu ya dizeli na mafuta ya taa: Sh227.98 na Sh220.12 kwa lita, mtawalia.
Nakuru iko katikati, ikiwa na petroli kwa Sh225.85, dizeli Sh227.17 na mafuta ya taa Sh219.30 kwa lita. Kisumu na Eldoret zina bei zinazofanana: petroli Sh226.62, dizeli Sh227.98 na mafuta ya taa Sh220.12.
Tofauti kati ya Mombasa na miji yenye bei za juu inatokana kwa kiasi kikubwa na gharama za kusafirisha mafuta kutoka pwani hadi maeneo ya ndani, kwa bomba na barabara. Kwa petroli, tofauti hiyo ni takriban Sh3.15 kwa lita; kwa dizeli ni Sh3.37 na kwa mafuta ya taa Sh3.41.
Hata hivyo, kwa mmiliki wa gari lenye tanki la lita 50, kujaza petroli kunagharimu takriban Shilingi 11,190 Mombasa, ikilinganishwa na Shilingi 11,348 Nairobi na Sh11,331 Kisumu. Hiyo ina maana kuwa dereva wa Nairobi analipa karibu Shilingi 158 zaidi ikilinganishwa na yule wa Momba, kwa tenki moja,
EPRA hutangaza viwango vya juu vinavyoruhusiwa kwa miji mingi zaidi ya hii mitano. Madereva katika maeneo mengine wanashauriwa kuangalia ratiba kamili ya mamlaka hiyo ili kujua bei inayotumika katika miji wao.
Viwango vilivyotangazwa ni ukomo wa juu, si bei ya lazima kwa kila kituo. Wauzaji wanaweza kuuza chini ya ukomo huo. Pia, madereva wanapaswa kutofautisha bei za rejareja wanazolipa pampuni na viwango vya jumla, ambavyo huwa chini. Kwa mfano, ukomo wa jumla wa petroli ya super Mombasa ni Sh208.73 kwa lita.
Ingawa tofauti ya bei kati ya miji ni ya gharama chache kwa lita huku ongezeko la mwezi huu likionekana kuathiri watumiaji kote nchini. Kwa kaya zinazotumia mafuta ya taa, na madereva wanaojaza mara kwa mara, gharama ya juu inaweza kuonekana haraka katika bajeti ya kila siku.

Hata hivyo baadhi ya watumiaji wa magari katika maeneno mbalimbali ya miji nchini, wamebaki na sitofahamu hususan wanaofanya biashara ya uchukuzi, wakishindwa namna ya kuendesha biashara hiyo.