Hali ya sintofahamu inaendelea kujikuza katika Kisiwa cha Amu, Kaunti ya Lamu, kufuatia mfululizo wa mashambulizi dhidi ya maafisa wa polisi na visa vitatu ambapo vijana wanaoshukiwa kujihusisha na uhalifu wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Visa hivyo vimeibua hofu kuhusu usalama wa maafisa wa usalama na wakazi, huku taarifa zikidai kuwa baadhi ya vijana wakibeba silaha butu na kukabiliana na maafisa wa usalama.
Maafisa wawili wa polisi wanaripotiwa kushambuliwa katika kipindi hicho. Tukio la hivi karibuni linamhusu Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCS) cha Kisiwa cha Amu, Mohammed Hassan Noor, ambaye alikatwa usoni kwa panga wiki iliyopita.
Shambulizi hilo linaangazia hatari zinazowakabili maafisa wa polisi wanapokabiliana na vitisho vya usalama na kuchunguza shughuli zinazoshukiwa kuwa za uhalifu.
Katika tukio jingine lililotokea mwezi uliopita, afisa mmoja wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) anaripotiwa kushambuliwa kwa kisu, hali iliyozidisha wasiwasi kuhusu ongezeko la visa vya vurugu dhidi ya maafisa wa usalama.
Vijana hao watatu walipigwa risasi na polisi katika matukio tofauti baada ya kudaiwa kujaribu kuwashambulia maafisa hao.
Hata hivyo, maelezo zaidi kuhusu mazingira ya kila tukio la ufyatuaji risasi, utambulisho wa waliohusika na iwapo uchunguzi rasmi umeanzishwa hayakuwa yamebainika.
Kutokana na hali hiyo, wito umetolewa kwa wakazi kushirikiana na vyombo vya usalama ili kukabiliana na uhalifu na kuzuia makabiliano zaidi kati ya vijana na polisi.
Aidha wananchi amewahimizwa kushirikiana kwa ukaribu na maafisa wa usalama katika kukabiliana na tatizo la vijana wanaodaiwa kutembea wakiwa wamejihami kwa silaha butu.
Aidha ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kuwabaini watu wanaoshukiwa kujihusisha na uhalifu na kuyasaidia mashirika ya usalama kuchukua hatua kabla hali haijazidi kuwa mbaya.
Wakazi pia wamehimizwa kuripoti shughuli zinazotia shaka na kuwapa mamlaka taarifa muhimu badala ya kuruhusu tofauti na makabiliano kugeuka kuwa matukio yanayoweza kusababisha vifo.
Visa hivyo vinajiri huku kukiwa na wasiwasi kuhusu usalama wa maafisa wa polisi na umuhimu wa kudumisha sheria na utulivu katika Kisiwa cha Amu, makazi ya kihistoria katika Kaunti ya Lamu.
Ushirikiano kati ya jamii na polisi unatarajiwa kuwa muhimu katika kukabiliana na changamoto hizo, kulinda wakazi na kuzuia mashambulizi zaidi dhidi ya maafisa wa usalama.
Hata hivyo, mamlaka zinatarajiwa kubaini mazingira halisi ya mashambulizi na matukio ya ufyatuaji risasi ili kurejesha imani ya umma na kuimarisha usalama katika eneo hilo.









