Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amefanya mkutano wa faragha na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na mwenzake wa Nyandarua John Methu.

Mkutano huo umefanyika eneo la Wamunyoro, Kaunti ya Nyeri,baadabya ziara ya Linda Mwanchi.

Mkutano huo unajiri wakati ambapo shughuli za kisiasa nchini zinaendelea kushika kasi, huku viongozi kutoka maeneo mbalimbali wakiongeza mikutano na mashauriano kuhusu mwelekeo wa siasa za Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Gachagua, ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa serikali ya Rais William Ruto, amekuwa akijitahidi kuimarisha ushawishi wake wa kisiasa kupitia mikutano na viongozi wanaoshiriki katika mijadala kuhusu utawala, uwajibikaji na masuala yanayowaathiri wananchi.

Kukutana kwake na Sifuna, ambaye pia ni kinara wa chama cha Equitable Party,kunavutia hisia za kisiasa kutokana na nafasi ya seneta huyo katika siasa za upinzani na mijadala kuhusu mustakabali wa uongozi nchini.

Kwa upande wake, Seneta John Methu amekuwa akihusishwa na mrengo wa kisiasa unaomuunga mkono Gachagua, hasa katika juhudi za kuimarisha ushawishi wa viongozi wanaopinga baadhi ya sera za serikali ya sasa.

Ziara ya Linda Mwananchi, ambayo imehusisha mikutano ya kisiasa na mazungumzo kuhusu changamoto zinazowakabili wananchi, imekuwa sehemu ya shughuli za viongozi wanaotaka kujenga uhusiano wa karibu na wapiga kura.

Hata hivyo, haijabainika mara moja ajenda kuu ya mkutano wa faragha uliofanyika Wamunyoro, wala iwapo viongozi hao walijadili uwezekano wa kushirikiana kisiasa katika maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.

Pamoja na ziara za vuguvugu la linda Mwananchi,kumekuwa na cheche za maneno dhidi ya rais William Ruto na seneta huyo wa Nairobi kuhusiana na uhalali wa miradi ya maendeleo ambayo kwa hatua fulani wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanasema ili serikali ipige hatua, ni lazima iwajibishwe.

Aidha muungano wa upinzani pia unafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba rais Ruto hapati nafasi ya kurejea ikulu wakati Ruto akidai kwamba upinzani lazima ujifunze namna ya kuuza sera zake kwa wananchi na sio maneno matupu huku akinukuu baadhi ya wanasiasa na kauli zao za upande mmoja.