Mamlaka ya mapato nchini Kenya (KRA) imekamata simu 52 na kamera za kupaa maarufu kama Drones tatu katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi.
Ni katika operesheni inayolenga kukabiliana na juhudi za kuingiza bidhaa nchini kwa njia zisizo halali.
Bidhaa hizo ziligunduliwa wakati maafisa wa forodha walipokuwa wakikagua mizigo ya abiria walioingia nchini.
Aidha,maafisa hao walimtia shaka mfanyakazi mmoja wa usafi katika uwanja huo, alipokuwa akitoka katika jengo la abiria akiwa na mabegi mawili.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na KRA Jumamosi, Oktoba 17, 2026, mfanyakazi huyo alijaribu kutoroka baadabya kubaini kwamba maafisa wamegundua jambo lisilo la kawaids, inagwa juhdu zake zilihonga mwamba.
Wakati wa mahojiano, mfanyakazi huyo aliwaambia maafisa kuwa abiria mmoja wa kike ndiye aliyemkabidhi mabegi hayo na kumtaka ayapitishie eneo la ukaguzi wa forodha.
Maafisa walikagua mabegi hayo kwa kutumia mashine ya kisasa ya kuchanganua mizigo aina ya Computerised Tomography (CT), iliyofichua uwepo wa drones pamoja na simu mbalimbali za mkononi.
Baadaye, maafisa hao walimtafuta abiria huyo wa kike, ambaye alikuwa amewasili nchini kwa ndege ya kimataifa.
Mshukiwa ,alithibitisha kuwa alimkabidhi mfanyakazi huyo mabegi hayo alipokuwa akitumia vyoo vya uwanja wa ndege.
Uchunguzi wa nyaraka zake za usafiri ulionyesha kuwa alikuwa msafiri wa mara kwa mara. Hali hiyo iliwafanya maafisa kufanya ukaguzi wa kina wa mizigo hiyo mbele ya abiria huyo na mfanyakazi wa uwanja wa ndege.
Ukaguzi huo ulibaini kuwa mabegi hayo yalikuwa na simu 52 zilizopig2a rangi na kurejeshwa sokoni, drones tatu, na baadhi ya bidhaa vinavyoendana na mali
Miongoni mwa vifaa vilivyokamatwa ni drones mbili aina ya DJI Mini 3 Pro, zikiwa na vidhibiti viwili na betri mbili, huku nyingine ikiwa aina ya DJI Air 2S, iliyokuwa na kidhibiti chake, betri na vifaa vingine.
Vifaa vingine vilivyopatikana ni chaja za simu, adapta za umeme za safari, nyaya za USB, vioo vya kinga ya uso za simu pamoja na mali binafsi.
KRA ilisema bidhaa hizo zimehifadhiwa katika ghala la forodha zikisubiri hatua zaidi za kisheria na kiutawala.
Mamlaka hiyo ilisisitiza kuwa tukio hilo linaonyesha umuhimu wa teknolojia ya kisasa ya ukaguzi wa mizigo katika kubaini bidhaa zinazoweza kufichwa au kupitishwa nchini kupitia njia zisizoidhinishwa.
KRA iliongeza kuwa inaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia na ukaguzi wa abiria unaozingatia viashiria vya hatari, kwa lengo la kurahisisha safari na biashara halali huku ikikabiliana na wanaojaribu kukwepa taratibu za forodha.
Katika taarifa yake, mamlaka hayo pia iliwakumbusha wasafiri na waagizaji kuwa kuingiza ndege zisizo na rubani nchini Kenya kunadhibitiwa na kanuni maalumu, na kunahitaji vibali husika kutoka kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (KCAA).
Wasafiri wanaonuia kuingiza vifaa hivyo nchini wametakiwa kuhakikisha wanatimiza masharti yote ya kisheria kabla ya kuvisafirisha hadi Kenya.
KRA ilisema itaendelea kulinda mapato ya serikali, kuimarisha usalama wa mipaka ya nchi na kurahisisha usafiri wa abiria wanaozingatia sheria kupitia matumizi ya teknolojia, taarifa za kiintelijensia na hatua za utekelezaji wa sheria.
Tukio hilo linaangazia changamoto zinazowakabili maafisa wa forodha katika kufuatilia bidhaa zinazoingia nchini kupitia vituo vikuu vya kuingilia, hasa pale ambapo baadhi ya watu huenda wakajaribu kukwepa taratibu za ukaguzi kwa kuhamisha mizigo kati ya abiria na wafanyakazi wa viwanja vya ndege.
Hata hivyo, KRA haikubainisha iwapo mashtaka yalikuwa yamefunguliwa dhidi ya abiria huyo au mfanyakazi wa uwanja wa ndege kufikia wakati wa kutolewa kwa taarifa hiyo.









