Chama cha Madaktari nchini Kenya (KMA) kimetoa wito kwa Wizara ya Afya na washirika wake kuhakikisha wahudumu wa afya walioathiriwa na ugonjwa wa Ebola wanapata matibabu bora, ulinzi na msaada wa kisaikolojia.
Katika taarifa iliyotolewa Oktoba 19, 2026, KMA kilieleza wasiwasi wake kufuatia kuthibitishwa kwa maambukizi ya Ebola miongoni mwa wahudumu wa afya walio mstari wa mbele katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Chama hicho, kinachowakilisha madaktari nchini Kenya, kilisema kuwa maambukizi hayo yamezua hofu miongoni mwa wahudumu wa afya na familia zao, kikisisitiza kuwa kila mhudumu anastahili mazingira salama ya kufanyia kazi na kupata huduma bora kwa wakati.
KMA kiliitaka Wizara ya Afya kuhakikisha wahudumu walioathiriwa wanapimwa na kuelekezwa kupata matibabu haraka, huku wakipewa vifaa vya kutosha vya kujikinga dhidi ya maambukizi.
Aidha, chama hicho kilisisitiza umuhimu wa mafunzo endelevu kuhusu kuzuia na kudhibiti maambukizi katika vituo vya afya, pamoja na kutoa msaada wa kisaikolojia kwa wahudumu walioathiriwa na familia zao.
KMA pia kiliwataka wasimamizi wa vituo vya afya kuziba mianya ya kiusalama, kuimarisha mifumo ya kuripoti uwezekano wa kuambukizwa na kuhakikisha wahudumu wanahimizwa kutoa taarifa mapema bila kuadhibiwa.
Katika mwongozo wake, chama hicho kilisisitiza kuwa wahudumu wa afya wanapaswa kufuata kikamilifu maelekezo ya Wizara ya Afya kuhusu kuzuia na kudhibiti maambukizi.
Wahudumu wanaoshuku kuwa wameambukizwa wanapaswa kuripoti hali hiyo mara moja.
Wale wanaoanza kuonyesha dalili wanashauriwa kusitisha kazi, kuepuka kugusana na watu wengine na kutafuta uchunguzi wa haraka kupitia mifumo rasmi ya kukabiliana na dharura za afya ya umma.
Rais wa KMA, Dk. Ibrahim Matende, alisema chama hicho kinaendelea kusimama na wahudumu walioathiriwa, kikiahidi kutetea usalama wao, ustawi wao na upatikanaji wa huduma za afya katika kipindi hiki.
Alisisitiza kuwa wahudumu hao hawako peke yao, akitambua mchango na kujitolea kwao katika kuwahudumia wagonjwa licha ya hatari zinazowakabili.
Hadi kufikia sasa,Kenya imeripoti takriban visa vinane vya maradhi ya Ebola wakati wadau wakilaumu kwamba mamlaka zinajikongoja kuchukua hatua stahili dhidi ya kinga.









