Kesi ya ufisadi inayomkabili aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu, kuhusu zabuni ya barabara yenye thamani ya Sh588 milioni, itarejea mahakamani Jumanne, Oktoba 27, 2026.
Aidha hii itakuwa ni kwa maelekezo zaidi kuhusu hatua zitakazofuata.
Hii ni baada ya faili la kesi hiyo kuwasilishwa mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama Alhamisi, huku pande zinazohusika zikisubiri ufafanuzi kuhusu namna ya kutekeleza uamuzi wa Mahakama Kuu uliofuta kuachiliwa huru kwa Waititu na washtakiwa wenzake dhidi ya mashtaka ya utakatishaji fedha.
Mnamo Oktoba 14, 2026, Jaji wa Mahakama Kuu Rose Ougo alithibitisha hukumu ya hatia dhidi ya Waititu na wenzake katika kesi ya ufisadi, huku akibatilisha uamuzi wa awali uliokuwa umewaachilia huru dhidi ya mashtaka matatu ya utakatishaji fedha.
Uamuzi huo ulitokana na rufaa iliyowasilishwa na upande wa mashtaka kupinga hatua ya mahakama ya chini kuwaachilia huru washtakiwa dhidi ya mashtaka hayo.
Baadaye, kesi hiyo ilirejeshwa katika Mahakama ya Hakimu Mkuu inayoshughulikia kesi za ufisadi ili kuendelea na hatua za kusikiliza hoja za kupunguziwa adhabu na kutoa hukumu kuhusu mashtaka ya utakatishaji fedha.
Hata hivyo, hatua hiyo ilikwama baada ya upande wa utetezi kupinga utaratibu uliopendekezwa wa kutoa hukumu, ukisema kuwa washtakiwa walikuwa tayari wameachiliwa huru dhidi ya mashtaka hayo na mahakama ya chini.
Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Vincent Monda, ulipinga hoja hiyo na kusisitiza kuwa Mahakama Kuu ilikuwa imekubali rufaa ya Serikali na kuelekeza washtakiwa kurejea mbele ya mahakama ya hakimu kwa hatua zinazohitajika kabla ya hukumu.
Kutokana na tofauti hizo za kisheria, mahakama ilihitaji ufafanuzi zaidi kuhusu utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama Kuu kabla ya kesi kuendelea.
Kesi hiyo inahusiana na zabuni ya ujenzi wa barabara katika Kaunti ya Kiambu yenye thamani ya takribani Sh588.7 milioni, iliyohusu kubadilisha barabara za changarawe kuwa barabara za lami katika maeneo ya Thika, Limuru, Gatundu Kaskazini, Juja na Ruiru katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018.
Waendesha mashtaka wanahusisha zabuni hiyo na madai ya ukiukaji wa taratibu za ununuzi wa umma na matumizi ya fedha zilizohusishwa na kandarasi iliyotolewa kwa kampuni ya Testimony Enterprises Limited.
Mnamo Februari 2025, Waititu alihukumiwa kifungo cha miaka 12 jela au kulipa faini ya takribani Sh53.5 milioni baada ya kupatikana na hatia katika mashtaka yanayohusiana na ufisadi.n
Mahakama Kuu ilidumisha hukumu hiyo ya hatia na adhabu mnamo Oktoba 2026, huku pia ikibatilisha kuachiliwa huru kwa washtakiwa dhidi ya mashtaka ya utakatishaji fedha.
Uamuzi huo pia ulifuta masharti ya dhamana yaliyokuwa.









