Serikali ya Kenya imeimarisha juhudi za kudhibiti ugonjwa wa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo (BVD), baada ya kuthibitisha visa tisa vya ugonjwa huo nchini, huku mgonjwa mmoja akiripotiwa kufariki na wengine wanane wakiendelea kupokea matibabu.

Juhudi hizo zilijadiliwa katika kikao cha nane cha Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Ebola kilichofanyika leo chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu katika Wizara ya Afya anayeshughulikia Afya ya Umma na Viwango vya Kitaalamu, Mary Muthoni.

Kikao hicho kililenga kutathmini maendeleo yaliyopatikana katika kukabiliana na mlipuko huo na kuimarisha mikakati ya kuzuia maambukizi zaidi nchini.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na kikosi hicho, watu wote 135 waliotambuliwa kuwa na uhusiano na kisa cha awali wamefuatiliwa, huku kukiwa hakuna ushahidi wa maambukizi kusambaa katika jamii.

Aidha, sampuli zote 14 zilizopimwa kutoka kwa watu waliokuwa wametajwa katika tahadhari za kiafya katika maeneo mbalimbali nchini ndani ya saa 24 zilizotangulia zilipatikana kuwa hasi.

Hata hivyo, mamlaka za afya zinaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa watu wanaoshukiwa kuambukizwa, usimamizi wa wagonjwa na maandalizi ya vituo vya kutenga wagonjwa ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

Kikosi kazi pia kilipitia upatikanaji wa vifaa muhimu vya matibabu, mahitaji ya vituo vya kutenga wagonjwa na mikakati ya kutafuta rasilimali za kuendeleza operesheni za kukabiliana na mlipuko huo.

Serikali imesema hatua za uchunguzi na ufuatiliaji zinaendelea, huku watu wa kwanza waliokamilisha masharti ya ufuatiliaji wakitarajiwa kumaliza kipindi chao cha siku 21 na kurejea nyumbani kuanzia Jumapili, Oktoba 25, 2026.

Muthoni alisisitiza dhamira ya serikali ya kuzuia kuenea kwa Ebola kupitia ushirikiano wa idara zote za serikali pamoja na wananchi na wadau wengine.

Maradhi ya Ebola yameripotiwa kwa mara ya kwanza nhcini DRC,na hatimaye maeneo mengine barani Afrika ikiwemo Kenya.

Hata hivyo wizara ya afya na mamlaka nyingine zinapambana katika kuhakikiaha kwamba maradhi hayo yanadhibitiwa haraka iwezekanavyo.

Taarifa za hivi punde zinasema,nchini Nigeria pia kumeripotiwa kisa cha maradhi hayo hatari.

Iwapo mamlaka zitazembea kuchukua tahadhari ipasavyo,huenda kesi za mauti au vifo zitaendelea kuongezeka.