Kinara wa chama cha People's Liberation Party (PLP), Martha Karua, amejiweka mbele kama mgombea anayefaa zaidi kupeperusha bendera ya upinzani katika uchaguzi mkuu ujao 2027.

Aidha ameonya kuwa hatakubali kudhalilishwa na mwanasiasa yeyote ndani ya mrengo huo.

Karua ameyasema hayo, wakati akiongoza hafla ya ufunguzi wa afisi za chama cha PLP katika kaunti ya Kisii, ambapo pia amekutana na viongozi wanawake kujadili nafasi yao katika uongozi wa taifa.

Akizungumza na wanahabari, Karua amesema wakati umefika kwa wakenya kuzingatia uongozi wa wanawake na kuwapa nafasi sawa na wanaume kushiriki katika uchaguzi na kuwania nyadhifa mbalimbali za kisiasa.

Amesitiza kuwa demokrasia inapaswa kuhakikisha kila mwananchi anapata nafasi ya kuwania uongozi bila kubaguliwa kwa misingi ya jinsia, akiwahimiza wanawake kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika siasa za nchi.

Karua ameelezea kuwa wanawake wana uwezo wa kuongoza na kushiriki katika maamuzi muhimu yanayoathiri maisha ya wananchi, akisisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vinavyowazuia kufikia nyadhifa za juu za uongozi.

Kuhusu hali ya kisiasa ndani ya upinzani, Karua anasema hatakubali kudunishwa, kutishwa au kufanyiwa uonevu na mwanasiasa yeyote kutokana na misimamo yake ya kisiasa.

Ameweka msisitizo kuwa ushindani wa kisiasa unapaswa kuongozwa na kuheshimiana, mashauriano na misingi ya demokrasia badala ya vitisho au juhudi za kuwanyamazisha wanaoonekana kuwa na misimamo tofauti.

Kauli yake inajiri wakati ambapo suala la umoja wa upinzani na namna ya kupata wagombea watakaowakilisha mrengo huo katika uchaguzi mkuu ujao ni miongoni mwa masuala yanayozingatiwa katika siasa za Kenya.

Karua pia ameelezea imani yake kuwa anafaa zaidi kupeperusha bendera ya upinzani, akionyesha azma yake ya kushiriki katika kinyang'anyiro cha uongozi wa kitaifa.

Hata hivyo, nafasi ya mwisho ya mgombea wa upinzani itategemea mashauriano na taratibu zitakazokubaliwa na vyama na viongozi wanaounda mrengo huo.

Ufunguzi wa afisi za PLP katika kaunti ya Kisii unalenga kupanua shughuli za chama hicho na kuimarisha uwepo wake katika eneo hilo, huku mkutano na viongozi wa wanawake ukitoa nafasi ya kujadili ushiriki wao katika siasa.

Kanrua amekuwa akishiriki katika siasa za Kenya kwa muda mrefu na amejijengea nafasi katika mijadala kuhusu demokrasia, utawala na usawa wa kijinsia.

Kupitia ujumbe wake, amesisitiza umuhimu wa kutoa nafasi kwa wanawake kuwania uongozi na kuhakikisha kuwa tofauti za kisiasa hazigeuzwi kuwa sababu ya vitisho au kudunishwa ndani ya upinzani.