Dar Es Salaam;Hukumu ya kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mawakili watatu wa mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo Chadema,Tundu Lissu, inatarajiwa kutolewa kesho Oktoba 16, 2026 na mahakama kuu, masjala kuu,Dodoma
Mwenyekiti huyo alikamatwa Aprili 9, 2025 akiwa kwenye mkutano wa hadhara wa chama chake na kufikishwa katika mahakam ya hakimu mkazi Kisutu, jijini Dar Es Saalam, na kusomewa kosa la uhaini.
Hadi sasa Lissu amekuwa gerezani kwa tuhuma hiyo ambayo ipo katika hatua ya mwisho kabla ya hukumu.
Aidha kesi hiyo ya kikatiba namba 7300/2026 inayotarajiwa kutolewa hukumu kesho Ijumaa, imefunguliwa na mawakili watatu, ambao ni Nashon Nkungu, Kulwa Maduhu na Paul Kisabo ambao wanajitambulisha kama washauri wa kisheria wa Lissu,katika kesi za jinai zinazomkabili.
Hata hivyo, walalamikiwa katika kesi hiyo ni mwanasheria mkuu wa serikali,kamishina mkuu wa magereza, mkuu wa gereza la Ukonga, Tundu Lissu na chama cha wanasheria Tanganyika (TLS) kilichounganishwa kama mdau mwenye maslahi.
Ingawa kesi hiyo iliyosikilizwa na jopo la majaji watatu, Amir Mruma, Dk Angelo Rumisha na Dk Everisto Longopa imefunguliwa mahakama kuu masjala kuu Dodoma, usikilizwaji wake utafanyika mahakama kuu masjala ndogo Dar Es Salaam na hukumu pia imepangwa kutolewa hapo.
Awali hukumu hiyo ilipangwa kutolewa Jumanne, Oktoba 13, lakini Jumatatu Mahakama hiyo ilitoa taarifa ya mabadiliko ya tarehe hiyo ya hukumu, kutoka tarehe hiyo ya awali.
Katika kesi hiyo mawakili hao walalamikaji,wanapinga vikwazo wanavyowekewa na mkuu wa gereza la Ukonga , kila wanapoenda gerezani kuzungumza na mteja wao, Tundu Lissu, anayehifadhiwa katika mahabusu ya gereza hilo kutokana na kesi ya uhaini inayomkabili.
Pamoja na mambo mengine, wanaiomba Mahakama itamke kuwa maofisa magereza kusikiliza mazungumzo yao na mteja wao ambaye ni Lissu,ni kinyume cha kanuni ya 13 ya kanuni za magereza , sheria na katiba kuhusu haki ya kusikilizwa kwa usawa na faragha na mteja wao.
Hata hivyo, mwanasheria mkuu wa serikali aliibua pingamizi la awali akidai kwamba kesi hiyo ni batili kwa kuwa wadaiwa wana njia mbadala za kupata nafuu (wanazoziomba) na hivyo kukiuka kifungu cha 8(2) cha sheria ya utekelezaji wa haki za msingi na wajibu.
Mahakama ilipanga kesi ya msingi Pamoja na pingamizi la awali la mwanasheria mkuu wa serikali kwa njia ya maandishi.









