Mwaka mmoja baada ya kifo chake
familia ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amolo Odinga, imewashukuru Wakenya waliojitokeza katika uwanja wa Migwena, Bondo, kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha kiongozi huyo mashuhuri wa kisiasa.

Kupitia ujumbe uliotolewa na Jaoko Oburu Odinga, familia hiyo imetambua mchango wa wananchi waliohudhuria hafla hiyo pamoja na wale waliofuatilia shughuli hizo kutoka majumbani mwao, ikisema mshikamano wao una maana kubwa katika kuendeleza kumbukumbu na urithi wa kisiasa wa Raila.

Jaoko alisema familia inathamini upendo na ushirikiano ulioonyeshwa na Wakenya katika kipindi hicho cha kumkumbuka aliyekuwa akijulikana na wafuasi wake kama Baba.

Ujumbe huo unajiri wakati familia, marafiki, wafuasi na washirika wa kisiasa wa Raila wanaendelea kutafakari mchango wake katika siasa za Kenya na safari yake ya muda mrefu ya kutetea mageuzi ya kidemokrasia.

Maadhimisho hayo katika uwanja wa Migwena yaliwakutanisha watu waliotaka kuheshimu kumbukumbu ya kiongozi huyo ambaye kwa miongo kadhaa alikuwa miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa katika siasa za taifa.

Kwa wafuasi wake, Raila alikuwa zaidi ya mwanasiasa; alikuwa ishara ya mapambano ya mageuzi, utetezi wa haki na msukumo wa mabadiliko ya kisiasa nchini Kenya.

Safari yake ya kisiasa iligubikwa na misukosuko, mapambano ya kisiasa na nyakati muhimu zilizochangia kuunda historia ya taifa, na kumfanya kuwa mtu mwenye wafuasi wengi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Shukrani za familia pia zinaangazia namna kumbukumbu ya Raila inavyoendelea kuwakutanisha Wakenya, licha ya tofauti zao za kisiasa na kijamii.

Katika ujumbe wake, Jaoko hakusita kutambua hata wale ambao hawakuweza kufika Bondo, lakini walitenga muda kufuatilia maadhimisho hayo wakiwa nyumbani.

Hatua hiyo inaonyesha kuwa familia inathamini kila namna ambayo wananchi wanaitumia kuendeleza kumbukumbu ya Raila na kuheshimu mchango wake kwa taifa.

Mwaka mmoja baada ya kifo chake, jina la Raila Odinga linaendelea kuwa sehemu muhimu ya mijadala kuhusu historia, demokrasia na mustakabali wa siasa za Kenya.

Hata hivyo,baadhi ya viongozi waliotarajiwa kuhudhuria sherehe hiyo,hawakufika licha ya kuwa ya kitaifa.