Maandalizi ya sherehe za kitaifa za Mashujaa Day katika Uwanja wa Kipchoge Keino mjini Eldoret yameongeza fursa za biashara na ajira kwa wakazi, huku serikali ikiimarisha usalama kuhakikisha hafla hiyo inaadhimishwa kwa amani.
Kamishna wa Mkoa wa Bonde la Ufa, Abdi Hassan, amesema vyombo vya usalama vimejiandaa kikamilifu kukabiliana na changamoto zozote zinazoweza kujitokeza wakati wa sherehe hizo.
Hassan amewaonya wananchi dhidi ya kutumia mazingira ya sherehe na shamrashamra zake kama fursa ya kukiuka sheria, akisema maeneo yote yanayoweza kuibua changamoto za usalama yamezingatiwa.
Wakati mipango ya usalama ikiendelea, shughuli za maandalizi katika uwanja huo zimeongeza idadi ya watu wanaofika eneo hilo, hali inayowanufaisha wafanyabiashara na kuwapa wafanyakazi nafasi za kujipatia kipato.
Akizungumza katika Uwanja wa Kipchoge Keino, Marka Shalo, mmoja wa wafanyabiashara wanaonufaika na maandalizi hayo, alisema shughuli za kuelekea Mashujaa Day zimechangia kuimarika kwa biashara yake.
Kwa upande wake, Fatima Barbara alisema anafurahia kuona Eldoret, inayojulikana kama Home of Champions, ikipata fursa ya kuandaa sherehe muhimu za kitaifa.
Maandalizi hayo pia yamezalisha nafasi za ajira kwa wafanyakazi wanaohusika katika shughuli mbalimbali za kukamilisha maandalizi ya uwanja huo. Baadhi ya wafanyakazi wamesema kazi hizo zimewapa nafasi ya kupata mapato.
Wakazi pia wamepongeza juhudi za serikali za kuhakikisha uwanja huo unakamilika kwa wakati, huku wakimtaja Katibu Mkuu wa Wizara ya Utumishi wa Umma, Dkt. Raymond Omollo, kwa kutembelea eneo hilo mara kwa mara kukagua maendeleo ya kazi.
Wakazi wanatumai kuwa uwanja huo utaendelea kuwa na manufaa hata baada ya sherehe za Mashujaa Day, kwa kuvutia watalii, wageni wa kimataifa na mashindano makubwa ya michezo.
Baadhi yao pia wanatazamia uwezekano wa Eldoret kuwa mwenyeji wa mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mwaka 2027, wakisema hatua hiyo inaweza kuongeza shughuli za kibiashara na nafasi za ajira.
Huku maandalizi yakielekea kukamilika, wafanyabiashara na wafanyakazi wanatumai kuwa ongezeko la shughuli katika eneo hilo litaendelea kwa muda mrefu, huku usalama ukiendelea kupewa kipaumbele wakati wa hafla hiyo.









