Kampuni ya mawasiliano nchini Kenya,Standard Group PLC italazimika kufanya mageuzi ya uongozi baada ya Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wake, Chaacha Mwita, kusemekana kujiuzulu.
Mwita anaondoka katika nafasi yake ya mkurugenzi mtendaji, huku uamuzi huo ukianza kutekelezwa Novemba 1,mwaka huu 2026.
Katika taarifa kwa wadau mbalimbali na umma kwa ujumla wake, bodi ya kampuni hiyo ilimshukuru kwa kujitolea na mchango wake katika kipindi alichohudumu. Hata hivyo, haikueleza kiini kilichosababisha kujiuzulu kwake wala kumtaja atakayechukua nafasi yake.
Kuondoka kwa Mwita kunakuja miezi michache tu baada ya kuthibitishwa kuwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa kudumu, kuanzia Aprili 1 mwaka huu 2026.
Aidha alikuwa akiikaimu nafasi hiyo tangu Julai 2025, kufuatia kujiuzulu kwa mtangulizi wake, Marion Gathoga-Mwangi.
Kabla ya kuwa CEO, Mwita alikuwa Mhariri Mkuu wa Maudhui wa Standard Group, akisimamia utayarishaji wa maudhui na kuchangia katika mikakati ya uhariri na uendeshaji wa kampuni.
Bodi ilipomthibitisha katika nafasi hiyo ya kudumu, ilisema tathmini yake ya utendakazi na mchakato wa uteuzi vilionyesha kuwa alikuwa na uwezo, uzoefu na uadilifu unaohitajika kuiongoza kampuni.
Mwita ana uzoefu katika uandishi wa habari, mawasiliano, uongozi na masuala ya sera. Amehudumu katika nafasi za uongozi katika Standard Group, Nation Media Group, Aga Khan Foundation, African Population and Health Research Centre na Thomson Foundation.
Ana shahada ya Elimu na stashahada ya uzamili katika Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, pamoja na shahada ya MBA kutoka Chuo Kikuu cha St Gallen nchini Uswisi.
Standard Group inaendesha gazeti la The Standard, vituo vya televisheni vya KTN, vituo vya redio na majukwaa ya habari ya kidijitali. Kuondoka kwa Mwita kunaongeza mabadiliko ya uongozi katika kampuni hiyo, ambayo inaendelea kukabiliana na mazingira yanayobadilika katika sekta ya habari.
Hata hivyo, katika siku kadhaa zilizopita, idadi kubwa ya vyombo vya Habari nhcini Kenya vimeshuhudiwa vikifanya mageuzi kadhaa, likiwemo la kuwapunguza wafanyakazi wake kutokana na madai ya kupanda kwa gharama za uendeshaji.Hali hiyo imesababisha ongezeko kubwa la waandishi wa habari kukosa ajira.









